Monday, August 7


Watu wengi ambao wamekuwa hawapigi hatua kwenye kazi zao, hasa wale ambao wameajiriwa, ni kwa sababu, wao wenyewe, bila ya kujua, wanakuwa wanahujumu kazi zao. Yaani kuna mambo wanafanya au kutokufanya, ambayo yanawapelekea kukosa fursa nzuri za kupiga hatua, kama kupandishwa cheo na kupewa majukumu zaidi.


Hujuma ambazo watu wamekuwa wanafanya kwenye kazi zao, hazitokani na wao kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi, bali zinatokana na tabia zao nyingine, nje ya majukumu yao ya kikazi. Pamoja na watu kuwa na ujuzi mzuri, akili nzuri ya kufanya mambo, zipo sifa nyingine muhimu zinazochangia mtu kufanikiwa. Wengi hupuuza sifa hizo, na kujikuta wakibaki pale pale, huku wengine wakipiga hatua.

Umewahi kuwa kwenye kazi, halafu wewe ukawa upo ngazi ile ile kila mwaka, huku watu wengine wanakuja na kukukuta wewe kwenye kazi, ila wanapanda ngazi na kukuacha wewe? Kama jibu ni ndiyo najua utakuwa unasema sababu ni upendeleo au wewe hujaliwi. Lakini ukweli ni mkubwa kuliko hivyo, kuna vitu unafanya, au kutokufanya ambavyo vinapelekea wewe kuachwa na wengine kupewa fursa zaidi.

Mshauri, mwanasaikolojia na mwandishi Lois Frankel, ametufunulia mambo hayo kwa kina kupitia kitabu chake hichi. Ni kitabu kizuri sana, ambacho kila mtu anapaswa kukisoma. Japo kimeandikwa kuwalenga watu wenye ajira, lakini kina mafunzo muhimu sana kwa kila mtu. Hata kwa walioajiriwa au wafanyabiashara, zipo sifa ukijifunza humu, zitakuwezesha kupiga hatua kubwa. Mimi binafsi yapo mambo nimejifunza ambayo sikuwahi kufikiria nguvu yake kama ilivyoelezwa, na ninaanza kuyafanyia kazi mara moja.

Karibu kwenye uhambuzi huu wa kitabu, nimekuandalia yale machache muhimu, utaendelea kujifunza zaidi kwa kusoma kitabu chenyewe.

1. Kama unaona umekwama kwenye kazi au chochote unachofanya, hiyo ni kwa sababu kuna sifa fulani ambazo unazikosa. Sifa hizo zinaweza zisiwe na uhusiano na kazi unayofanya, bali ikawa ni mahusiano yako na wengine, mwonekano wako, maongezi yako na kadhalika. Hivyo kabla hujaamini kwamba wengine wanapendelewa, angalia wapi unakosea kisha chukua hatua.

2. Katika kuchukua hatua ya kujijengea tabia bora kabisa za mafanikio kupitia kazi yako, usikimbilie kuangalia uache kufanya nini, badala yake angalia wapi upo imara, kisha angalia kipi cha kuongeza ili uweze kupiga hatua. Kwa mfano, watu wengi wanaweza kuwa ni wafanyakazi wazuri mno kwenye kazi zao, lakini hawawezi kuelewana na wengine vizuri, hilo linawanyima fursa ya kupandishwa cheo na kuwa wasimamizi. 

Ukigundua kwamba udhaifu wako uko hapo, unahitaji kujenga mahusiano yako na wengine ili kuweza kupiga hatua, huku ukiendelea kufanya kazi yako vizuri.

3. Tabia ulizojifunza ukiwa utotoni, zina mchango mkubwa wa hapo ulipo sasa. Kila mtu alipokuwa mtoto, kuna tabia alizojifunza, za kumwezesha kuishi kwenye hii dunia. Hizi ni zile tabia ambazo tulikuwa tunazo ili kuhakikisha tunapata kile ambacho tunakitaka. Tabia hizi huwa haziishii utotoni, bali zinaenda na sisi mpaka ukubwani. Iwapo hutazitambua tabia hizi na kuondokana nazo, huwezi kupiga hatua. Kwa mfano kama utotoni umekulia kwenye malezi ambayo wazazi walikuwa wakali sana, na hivyo ukahitaji kuwa mvumilivu na mpole mno, maisha yako yote utaenda na tabia hiyo. Sasa unaweza kuwa kwenye mazingira magumu sana ya kazi, lakini unashindwa kuchukua hatua, kwa sababu umezoea hivyo tangu utotoni. Unahitaji kuvunja tabia za utotoni ili kuweza kupiga hatua.

4. Wale wanaofanikiwa kwenye kazi zao, huwa wanayasoma mazingira ya kazi wanayofanya, na uongozi uliopo, kisha wanabadili tabia zao kuhakikisha zinaendana na mazingira yake. Kwa njia hii, wanaonekana kuweza zaidi kazi zao na kupewa majukumu zaidi. Wale wanaoshindwa, huwa wanang’ang’ana na kile wanachotaka wao, wakiona wana msimamo, na yale maeneo ambayo wana udhaifu, yanakuwa kikwazo kwao kupiga hatua.

5. Zipo tabia nane ambazo watu wamekuwa nazo, na zimekuwa zinawazuia kufanikiwa kupitia kazi zao. Tabia hizo ni kama ifuatavyo;

Moja; kutokujali watu wengine.

Mbili; kushindwa kufanya kazi kama timu.

Tatu; kushindwa kuwa na mawasiliano bora.

Nne; kukosa akili hisia (emotional intelligence)

Tano; kushindwa kufanya kazi na mamlaka.

Sita; kukosa maono au kuwa na maono mapana sana.

Saba; kushindwa kuwapa watu kile wanachotegemea.

Nane; kufanya kazi kwa kujitenga.

Zipo njia nane za kutengeneza mafanikio kwenye kazi yoyote ile. Tutakwenda kuziangalia hapa na hatua za kuchukua ili uweze kupiga hatua.

Njia ya kwanza; jenga mahusiano bora na wengine.

6. Tengeneza mahusiano yako na watu wengine ambao unafanya nao kazi. Kwa kujali kuhusu kazi zao na maisha yao kwa ujumla.

7. Wengine wanapoongea, sikiliza kwa makini, sikiliza kwa lengo la kuelewa na siyo kwa lengo la kubishana.

8. Yajue majina ya wafanyakazi wenzako na majina ya watu wao wa karibu. 

Unapoyatumia majina hayo watu wanaona unajali.

9. Waheshimu watu wote kwa usawa, iwe wapo juu yako au chini yako. Usimdharau mtu kwa sababu yupo chini, itakuja kukugharimu baadaye.

10. Soma kitabu cha Dale Carnegie kinachoitwa HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE.

Njia ya pili; kuwa mtu muhimu kwenye timu ya kazi.

11. Fanya kazi ndani ya timu, na chagua kitu ambacho unachangia kwenye timu. Hapa unaangalia kipi ambacho timu ya kazi inakutegemea, kisha kitoe vizuri.

12. Kuwa mtu rafiki kwa watu kuweza kufanya kazi na wewe, toa ushirikiano wa kutosha, kiasi kwamba ikitokea kazi ambayo watu wanapaswa kufanya kwa kushirikiana, basi kila mtu apende kushirikiana na wewe.

13. Wasaidie wengine kukamilisha majukumu yao, angalia ni namna gani unaweza kuwa na mchango zaidi kwenye kazi za wengine, na utoe.

14. Soma kitabu kilichoandikwa na Jon Katzenbach na Douglas Smith kinachoitwa THE WISDOM OF TEAMS.

Njia ya tatu; tengeneza mwonekano na mawasiliano yako.

15. Hakikisha unakuwa na mwonekano mzuri kwa wengine, mwonekano mzuri unakupa nafasi ya kufanikiwa zaidi. Kuwa na nguo za heshima na onekana nadhifu wakati wote.

16. Unapokuwa kazini, vaa kwa ile nafasi unayotaka kufikia, na siyo nafasi uliyopo sasa. 

Kwa mfano kama unataka kuwa meneja, angalia mameneja wanavaa mavazi ya aina gani, na vaa kama wao. Hata kama kazi yako ni ya chini kabisa. kwa kufanya hivyo, unatengeneza taswira ya umeneja ndani yako na itaonekana na wengine.

17. Mtindo wako wa kutembea na hata wa kukaa, uwe wa mtu anayejiamini na siyo kama wa kukata tamaa.

18. Mwili wako uwe na afya ya kawaida, uzito usiwe umezidi wala usiwe umepungua sana. Fanya mazoezi kuhakikisha unakuwa na afya bora.

19. Unapoongea, ongea kwa kujiamini, ongea kwa sauti inayosikika vizuri, na tumia maneno ambayo kila mtu anaweza kukuelewa.

20. Soma vitabu vitatu; THE DEFINITIVE BOOK OF BODY LANGUAGE, BUSINESS CLASS; ETIQUETTE ESSENTIALS FOR SUCCESS AT WORK na SPEAK LIKE A CEO; SECRETS FOR COMANDING ATTENTION AND GETTING RESULTS.

Njia ya nne; boresha akili hisia yako (emotional intelligence).

21. Kamwe usimdhalilishe mtu yeyote mbele ya watu wengine, watu watakuchukia na kushindwa kushirikiana na wewe.

22. Wasifie watu hadharani, lakini wakosoe faragha, kwa njia hii watu watapenda kufanya kazi na wewe.

23. Kumbuka kusema tafadhali, asante na samahani kila linapohitajika neno la aina hiyo. 

Unataka mtu afanye kitu, anza na tafadhali. Kama mtu amekupa kitu au amefanya chochote, hata kama ni kidogo sema asante. Unapokosea sema samahani.

24. Kuwa mwaminifu, timiza kile unachoahidi.

25. Usifuate sheria ya dhahabu kwamba wafanyie wengine kile ambacho ungependa wakufanyie, badala yake fuata sheria ya almasi kwamba wafanyie wengine kile ambacho wanapenda kufanyiwa.

26. Soma vitabu viwili; THE EMOTIONAL INTELLIGENCE QUICK BOOK na THE LIKEABILITY FACTOR.

Njia ya tano; waongoze wanaokuongoza.

27. Kumbuka sheria ya dhahabu kwenye utawala, mwenye dhahabu ndiye anayepanga sheria. Hivyo chochote unachofanya, hakikisha walio juu yako wanajiona wapo salama na kuweza kukutegemea wewe.

28. Usijaribu kuonekana unaweza zaidi au kujua zaidi kuliko aliye juu yako, atatumia nafasi yake kukupoteza kabisa. Kila mtu anapenda kulinda nafasi yake.

29. Bosi wako siyo mzazi wako, elewa majukumu ya kila mmoja wenu na mwisho wa majukumu hayo. Usimng’ang’anie bosi, hasa pale anapoonekana kuwa msumbufu.

30. Makubaliano yakishafikiwa na uongozi, yasimamie hata kama ulikuwa unayapinga.

31. Kama unafanya kazi chini ya mtu asiyekujali, anayekutumia na kukudharau, unapaswa kuchukua hatua ya kutafuta nafasi nyingine, unaweza kusubiri ukiamini mambo yanabadilika, ila ni mara chache sana mambo hubadilika.

32. Soma kitabu; YOUR BOSS IS NOT YOUR MOTHER

Hizi ni njia tano kati ya njia nane za kufanyia kazi ili kuweza kupiga hatua kwenye kazi yako. Nakushauri sana usome kitabu hichi, kwa sababu utajifunza mengi mno, hasa jinsi ya kuboresha mahusiano na wengine, kuweza kufanya kazi na wengine, na hata kujua namna gani ya kupendwa na wengine.

0 comments:

-