Kama leo ungekutana na mtu njiani akakuuliza kama unapenda
kuwa mzee ungemjibu vipi. Nina hakika ungejibu ndiyo au hapana. Hebu
nikufahamishe ugunduzi wangu. Kabla ya kuandika makala hii niliwauliza
watu wengi swali hili kwa lengo la kujua watu wanapenda kiasi gani uzee.
Kwa
hakika watu wengi walisema hawapendi uzee. Ni wachache waliosema
wanapenda kuwa wazee. Hata hao wachache nilipowadadisi zaidi ilionekana
hawakuwa thabiti katika majibu yao.
Kama wewe ni mmoja
wa wale ambao hawaupendi uzee usisikitike. Historia ya jitihada za watu
kutaka kubaki vijana ina muda mrefu karibuni sawa na historia ya
binadamu kuwa ulimwenguni. Tangu historia ilipoanza kuandikwa, binadamu
wamebainika kufanya mambo mbalimbali ili kubakia katika hali ya ujana.
Kuna waliovaa talasimu za aina mbalimbali, waliokwenda sehemu zenye
maajabu kama vile masinagogi, milima, majabali, mito na mapango ambako
ilisadikiwa kuwa wangerudi katika ujana, wangezuia wasizeeke na pengine
hata kuzuia kifo.
Kuna kisa cha mvumbuzi na jemedari
mashuhuri wa Hispania, aliyeitwa Juan Pance de Leone aliyefanya safari
ndefu kuvuka bahari hadi katika Bara la Amerika kwa ajili ya kufanya
uvumbuzi. Licha ya uvumbuzi alikuwa akitafuta chemichemi ya ujana ambayo
aliambiwa maji yake humrudisha mtu katika ujana. Alitangatanga hadi
mwaka 1513, akafika Florida kulikokuwa na chemchem hiyo. Hata hivyo
aligundua kuwa ulikuwa uzushi tu, maana maji hayo hayakumsaidia kutimiza
lengo lake.
Katika miaka michache iliyopita, kulikuwa na kisa kilichosambazwa mitandaoni kilichomuhusu binti fulani.
Binti
huyo alisafiri kwenda masomoni katika nchi fulani. Alipofika akawatumia
wazazi wake kichupa cha dawa nakuwaelekeza kila mmoja anywe tone moja
ili wasizeeke. Baada ya miaka ya kumi aliporudi alimkuta mama yake
amekuwa binti huku amebeba katoto ka kiume. Alifurahi kumkuta mama yake
amekuwa binti. Akamuuliza “Mama baba yuko wapi” mama akamjibu “Baba yako
alipoona nimekunywa tone na nimekuwa binti, badala ya kunywa tone, yeye
alikunywa kichupa chote, ndiyo huyu niliyembeba”.
Ingawa
kisa hiki kilikuwa cha kubuni tu watu wengi walikisadiki na wakaanza
kujiuliza ni nchi gani huyo, msichana alikokwenda na kupata dawa hiyo
iliyowapunguza umri wazazi wake.
Kuna watu wengi siku
hizi ambao wanatafuta na kuulizia aina za vidonge na toniki ambazo
zingewaweka katika hali ya ujana na furaha.
Hata hivyo
wameshindwa kutambua mienendo inayoathiri miili yao na kuifanya ichakae
haraka. Badala yake wanatumia fedha nyingi kwenye maduka ya dawa.
Ni
kweli kuwa vitamin na madini huboresha afya ya mwili wa binadamu.
Lakini hivi sivyo vitu pekee vinavyoweza kumfanya mtu awe kijana na
kutononeka.
Ingawa furaha iliyoje kama tungeweza kupata
ujana wa milele. Hivi leo kuna nadharia nyingi zinazofikiriwa kuwa
zingeweza kumsaidia mtu kumfanya awe kijana na mwenye afya bora.
Nadharia moja ya kibaolojia inadai kuwa mwili hubaki katika ujana
kutokana na viungo vya binadamu kama vile usawazisho wa homoni na
ukuwaji wa viungo, kama mishipa inayopelekea damu kwenye moyo na jinsi
utumbo mkubwa unaomengenyua viini lishe vilivyomo katika vyakula
tunavyokula.
Lakini siku hizi, madaktari wanakubaliana
na wanasaikoiojia kuwa “Mtu huzeeka kutokana na hisia zake”. Jambo hili
ni kweli kwa kuwa akili ina athari kubwa kwenye mwili mzima wa binadamu.
Ni vyema kuwa watu wengi hutamani ujana na kukataa uzee. Wanachohitaji
ni uwezo tu wa kuzifanya akili zao zisiwaeleke kujihisi kuwa wao ni
wazee, maana unapojivisha uzee kwa imani utakuwa mzee kweli hata kama
umri wako ni mdogo. Kuna usemi mmoja wa kingereza usemao”No one gets too
old to feel young” yaani hakuna anayezeeka sana hadi akashindwa
kujisikia kuwa ni kijana. Mpaka sasa tumegundua kuwa kuna sababu za
kibaolojia na za kisaikolojia zinazoweza kutufanya tuendelee kuwa katika
hali ya ujana. Tukiwa makini katika kuipatia miili yetu matunzo mazuri
na aina sahihi za vyakula tutasababisha msawazisho mzuri wa homoni,
mishipa ya damu itabaki katika hali ya uchanga na kuweza kunyumbulika na
kuufanya mfumo wa kumeng’enyua chakula mwilini ukafanya kazi vizuri,
tutaendelea kuwa vijana kwa muda mrefu zaidi katika maisha yetu.
Aidha,
daima tukumbuke kuwa matunzo ya mwili, ulaji mzuri wa chakula, kupata
usingizi na mapumziko ya kutosha pamoja na mazoezi, ndivyo
vitakavyoufanya ubongo uwe katika hali nzuri ya kuuwezesha kuhisi ujana
kwa ufanisi mkubwa zaidi. Katika suala la kudumisha ujana na uchangamfu
wa mwili kilicho muhimu siyo kufikiria tumeishi miaka mingapi, wala
kutazama kalenda na kuhesabu siku, majuma na miezi, bali ni kujiuliza
tumeishi namna gani na tumejifunza kiasi gani jinsi ya kuziongoza hisia
zetu kuelekea katika msimamo wa ujana.
Maisha yenye
utomvu wa ujana hutegemea vitu viwili muhimu, ambavyo ni fizikiolojia
yenye maana ya jinsi mwili wa binadamu unavyofanya kazi vyema kwa
kuhusianisha viwiliwili vyote katika hali ya kufanya kazi sawasawa.
Kitu
kingine kinachohusiana na mwenendo wa mwili kubaki katika hali ya ujana
ni kifiziolojia, yenye maana ya akili iliyotamalaki sawasawa kwa kuweza
kudumisha hisia ya uhai na uzima bila kujali ni miaka mingapi ambayo
mtu ameishi.
0 comments:
Post a Comment