Thursday, January 14


glo-awards 2015
Tuzo za mchezaji bora wa mwaka za CAF zinatimiza miaka 24 mwaka huu tangu kuanzishwa kwake ambapo leo January 7, 2016 sherehe za ugawaji tuzo hizo zinafanyika kwenye jiji la Abuja, Nigeria.
Leo mfalme wa soka la Afrika atakabidhiwa tuzo yake kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa Abuja ambapo Yaya Toure ambaye ni mshindi wa tuzo hiyo mara nne mfululizo, mshambuliaji wa kimataifa wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang na mghana Andre Ayew, mmoja kati yao atatangazwa mshindi.
Samuel Eto’o alikuwa ni mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo mara nne hiyo ilikuwa ni mwaka 2003, 2004, 2005 na 2010 rekodi ambayo imefikiwa na Yaya Toure ambaye ametwaa tuzo hiyo mara nne mfululizo (2011, 2012, 2013 na 2014). Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Senegal El HadjiDiof alishinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo mwaka 2001 na 2002.
Hata hivyo, mchezaji wa kwanza kuwahi kutwaa tuzo hiyo mara mbili kwa vipindi tofauti alikuwa ni Nwankwo Kanu ambaye alichukua mwaka 1996 na 1999 kabla ya Mu-Ivory Coast Didier Drogba kuibeba mara mbili pia mwaka 2006 na 2009.
Washindi wa tuzo hiyo mara zote wamekuwa ni viungo au washambuliaji na utamaduni huo umeendelea tena mwaka huu kutokana na majina yaliyoingia fainali kuwania tuzo hiyo kuwahusisha wachezaji wa sekta hiyo.
Kwa nyongeza, wachezaji 14 ambao wamefanikiwa kuinyakua tuzo hiyo tangu mwaka 1992 wamekuwa ni mabalozi wazuri wa Afrika duniani kote wa mchezo huo unao-ongoza kwa kuwa na mashabiki wengi.
Walikuwepo pia wachezaji kadhaa maarufu ambao walikaribia kuichukua tuzo hiyo lakini hawakufanikiwa kufanya hivyo, golikipa wa Ivory Coast Alain Gouamene mwaka 1992, beki wa Morocco Nourreddine (alimaliza akiwa nafasi ya sita mwaka 1993), M-Nigeria Daniel Amokachi ambaye mara kadhaa jina lake lilikuwa likiishia kwenye top ten.
Beki wa Afrika Kusini Mark Fish alimaliza akiwa nafasi ya sita mwaka 1996. Samuel Kuffour beki wa Ghana aliikosa tuzo hiyo kwa miaka miwili tofauti, mwaka 1999 na mwaka 2001. M-Ghana Michael Essien ambaye kwa mara tano mfululizo alikuwa akiishia nafasi ya tatu kuanzia mwaka 2005, 2006, 2007, 2008 na 2009.
Asamoah Gyan pia kutoka Ghana mwaka 2010 alimaliza katika nafasi ya pili wakati Andre Ayew alimaliza katika nafasi ya tatu kwenye tuzo za mwaka 2011. Seydou Keita alimaliza nafasi ya pili mwaka 2011 wakati Wanigeria wawili John Obi Mikel na Vincent Enyeama walimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu mwaka 2013 na mwaka 2014 kila mmoja kwa mfuatano.
Wakati muda mchache ukiwa umesalia mshindi wa tuzo hiyo kutangazwa, kuna kitu muhimu ambacho watu wengi inabidi wafahamu.
Ivory Coast ni taifa ambalo lina idadi kubwa ya tuzo hiyo. Ivory Coast imefanikiwa kushinda tuzo hiyo mara sita kwa ujumla, Toure ameipeleka tuzo hiyo nchini kwao (mara nne) na Drogba (mara mbili) ikifuatiwa na Nigeria ambayo imetwaa taji hilo mara tano Kanu (mara mbili), Emanuel Amunike, Rashid Yekini na Victor Ikpeba wote mara mojamoja.
Patrick Mboma ametwaa tuzo hiyo mara moja wakati Eto’o ameshinda tuzo hiyo mara nne na kuifanya Cameroon kutwaa tuzo hiyo mara tano. Diouf ameshinda tuzo hiyo mara mbili na kuifanya nchi yake ya Senegal kutwaa tuzo hiyo mara mbili. Walionyakua tuzo hiyo mara moja ni pamoja na Abedi Pele wa Ghana, George Weah kutoka Liberia (mchezaji pekee aliyewahi kushinda tuzo ya FIFA Ballon d’Or) Mustapha Hadji wa Morocco, Frederic Kanoute wa Mali na Emanuel Adebayor wa Togo.
Kwa miaka tisa iliyopita, tuzo hizi zimekuwa zikidhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi (Globacom) ambao wameongeza heshima ya tuzo hizo kila zinapotolewa kwenye majiji kama Abuja, Accra, Lome, Lagos pamoja na Cairo.
Mwaka huu sherehe za ugawaji wa tuzo zitafanyika Abuja kwa mara ya pili tangu zilipofanyika kwa mara ya mwisho kwenye mji huo mwaka 2004.
Orodha ya wachezaji waliowahi kutwaa tuzo hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 1992:
1992 Abedi Ayew Pelle (Ghana)
1993 Rashidi Yekini (Nigeria)
1994 Emanuel Amunike (Nigeria)
1995 George Weah (Liberia)
1996 Nwakwo Kanu (Nigeria)
1997 Victor Ikpeba (Nigeria)
1998 Mustapha Hadji (Morocco)
1999 Nwankwo Kanu (Nigeria)
2000 Patrick Mboma (Cameroon)
2001 El-Hadji Diouf (Senegal)
2002 El-Hadji Diouf (Senegal)
2003 Samuel Eto’oo (Cameroon)
2004 Samuel Eto’oo (Cameroon)
2005 Samuel Eto’oo (Cameroon)
2006 Didier Drogba (Ivory Coast)
2007 Frederick Kanoute (Mali)
2008 Emanuel Adebayor (Togo)
2009 Dider Drogba (Ivory Coast)
2010 Samuel Eto’oo (Cameroon)
2011 Yaya Toure (Ivory Coast)
2012 Yaya Toure (Ivory Coast)
2013 Yaya Toure (Ivory Coast)
2014 Yaya Toure (Ivory Coast)


0 comments:

-