Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali iliyopita,
Bernard Membe ameungana na waziri mwenzake wa zamani, Dk Makongoro
Mahanga kukosoa sera ya kubana matumizi ya Rais John Magufuli ya
kudhibiti safari za nje na kuteua baraza dogo la mawaziri.
Kama ilivyokuwa kwa Dk Mahanga, waziri huyo aliyedumu kwa miaka tisa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje amesema kiuhalisia, Rais
hajapunguza idadi ya wizara kama alivyosema bali amepunguza “idadi ya
mifuko”, huku akisisitiza kuwa mkuu huyo wa nchi atalazimika kutoka nje
“atake asitake”.
Membe
amekuwa waziri wa pili wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukosoa sera
ya kubana matumizi ya Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Dk Mahanga,
ambaye sasa amehamia Chadema, kumkosoa akisema idadi ya wizara inapimwa
kwa kuangalia makatibu wakuu na si wizara na hivyo ukubwa wa Baraza la
Mawaziri bado uko palepale.
Akiongea
na Gazeti la Mwananchi, Membe alikuwa na maoni kama hayo na akaenda
mbali zaidi kuzungumzia hata sera ya kudhibiti safari za nje na Rais
kujizuia kusafiri, akisema “Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa” katika
dunia ya leo.
Membe,
ambaye alikuwamo kwenye kinyang’airo cha urais na kufika hadi tano
bora, alisema Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa
Baraza la Mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na
siyo wizara.
“Alichofanya
ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko
kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema Membe.
“Lakini
unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai
matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na
yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na
mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa
hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai.”
Rais
aliahidi kwenye kampeni na hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge kuwa
atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kubana matumizi. Alitekeleza
ahadi yake kwa kuunda baraza lenye mawaziri 34 tofauti na lililopita
ambalo lilikuwa na mawaziri 55.
Upunguzaji
huo wa baraza ulifanywa kwa kuunganisha wizara na hivyo kufanya
makatibu wakuu, ambao ni maofisa masuhuli wa wizara kuwa zaidi ya mmoja
kwenye baadhi ya wizara.
“Ameendeleza
wizara zilezile, lakini akaamua kuzikusanya pamoja. Hiyo haimaanishi
kuwa atakuwa amepunguza gharama za uendeshaji wake,” alisema Membe.
“Hilo
tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti
itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama
tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki
vilevile maana yake hakuna kilichofanyika.”
Membe
alitoa mfano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ambayo sasa inaitwa “Wizara ya Mambo ya Nje, Kikanda na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki”, akisema itapaswa kuwa na bajeti mbili; ya Mambo ya
Nje na Bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kinyume chake
ni vigumu kuiendesha.
Membe
alikiri kuwa hata yeye angeingia kwenye mtego wa kupunguza idadi ya
wizara kama angefanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais kama ilivyokuwa nchini
Namibia ambako wizara zilipunguzwa kutoka 32 hadi 20.
“Baadaye nikagundua kuwa hata Namibia yenyewe inajuta,” alisema.
Alisema
siku ya kuapishwa Rais Magufuli, alikutana na Makamu wa Rais wa
Namibia, Nickey Lyambo na baada ya kusalimiana na kumpongeza kwa hatua
ya kupunguza wizara, kiongozi huyo wa Taifa hilo la kusini mwa Afrika
alimweleza kuwa uamuzi huo umewasababishia matatizo makubwa bungeni
“Aliniambia katika Bunge la Namibia kuna mjadala mkali wa kutaka wizara ziongezwe,” alisema Membe akimnukuu makamu huyo wa rais wa Namibia.
Membe
alibainisha kuwa kwa Tanzania, mfumo huo mpya wa wizara pia unaweza
kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa kuwa mawaziri sasa
watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali ili kuzungumzia
wizara kadhaa zilizounganishwa, jambo ambalo lililalamikiwa pia na
kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu.
“Kila
kitu kina form na content (muundo na maudhui). Alichofanya Rais
Magufuli ni kubadili form na siyo content ya wizara, wizara ni zilezile
na mzigo ni uleule,” alisema.
Mbunge huyo wa zamani wa Mtama mkoani Lindi, pia alikosoa udhibiti wa safari za nje, akisema Tanzania si kisiwa.
Alikuwa
akijibu swali lililomtaka aeleze uhalisia wa mpango wa Rais Magufuli
kubana matumizi kwa kufuta safari za nje za mawaziri na watumishi
wengine wa umma.
Mara
tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alifuta safari zote za
nje ya nchi kwa watendaji na watumishi wa umma, isipokuwa zile tu ambazo
zingepata kibali cha Ikulu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kubana
matumizi ya Serikali.
Rais
Magufuli alisema katika hotuba yake ya kuzindua Bunge kuwa kuanzia
mwaka 2013 hadi 2015, safari hizo ziliigharimu Serikali Sh356.3 bilioni
na kwamba kati ya fedha hizo, Sh183.1 bilioni zilitumika kwa ajili ya
tiketi za ndege, Sh68.6 bilioni kwa ajili ya mafunzo na Sh104.5 bilioni
kwa ajili ya posho.
Bila kugusia madhara ya kufuta safari hizo, Rais Magufuli alijielekeza zaidi kwenye matumizi ya fedha ambazo angeokoa.
“Lakini
tujiulize fedha hizo zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? Zingeweza
kutengeneza nyumba za walimu ngapi? Zingeweza kutengeneza madawati
mangapi? Zingeweza kununua dawa hospitalini tani ngapi?” alihoji Rais Magufuli katika hotuba yake iliyotoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Lakini
Membe, ambaye wizara yake iliwahi kutetea safari za Jakaya Kikwete nje
ya nchi baada ya wapinzani kusema ziligharimu zaidi ya Sh4 trilioni,
alisema safari za nje zina umuhimu kwa taifa lolote.
“Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe ambaye ana shahada ya umahiri ya uhusiano wa kimataifa aliyoipata Marekani.
“Lazima
utakwenda mwenyewe au mawaziri wako na hasa Waziri wa Mambo ya Nje kwa
sababu kuna vikao nje ya nchi ambavyo mabalozi hawaruhusiwi kuingia.
“Ukijaribu kujifanya kisiwa utakuwa kama Zimbabwe. If you isolate yourself you will be isolated (ukijitenga, utatengwa).”
Membe
alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194
zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi
kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua
ya uamuzi watazuiwa kushiriki.
“Kwa
mfano, Uturuki hatuna ubalozi, sasa unapoona ndege inaleta watalii
kutoka Uturuki, unadhani Bunge la Uturuki liliketi kutuletea watalii
Tanzania? Hapana. Tulitoka nje na kuwashawishi wakaja,” alisema
Membe aliyewahi kueleza kuwa wakati wa awamu ya Rais Jakaya Kikwete
mawaziri walikuwa wanapishana angani kana kwamba kuna moto ardhini.
“Pia,
leo unaposikia gesi, gesi, gesi nayo imepatikana nje ya ubalozi.
Mawaziri walitoka nje ya nchi wakatafuta wawekezaji. Ni kazi ya wizara
kufanya yote hayo.”
Membe
alirudia kauli aliyoitoa siku chache kabla ya kuanza mchakato wa
Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa lazima waziri wa mambo ya nje awe nje ya
nchi kwa muda mwingi na ikitokea yuko ndani ya nchi kwa mwezi mmoja
mfululizo, lazima ni mgonjwa.
0 comments:
Post a Comment