Friday, November 27


Serikali imekanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa amekomba fedha hazina na kuiacha Serikali bila fungu lolote.
Hayo yamesemwa jijini dare es salaam na Kamishina wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha Bwa. John Cheyo huku akiwataka wananchi kupuuza habari hiyo kwani hazina ukweli wowote.
“Hazina inazo pesa za kutosha  na tunajivunia kufanya uchaguzi wa mwaka huu,  kununua mashine za BVR  kwa kutumia pesa za watanzania bila kutegemea msaada wowote kutoka nje ya nchi  na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka huu” alisema Bwa. Cheyo.
Pia aliongeza kuwa serikali imeendelea kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi ambalo limekamilika hivi karibuni, vinu vya kuchakata gesi na ujenzi wa barabara nchini.
Aliendelea kusema kwamba mfumo wa serikali wa bajeti unaiwezesha serikali kupanga vipaumbele vya matumizi kulingana na bajeti ilivyopangwa ambapo fedha zinazokusanywa kupitia mfuko mkuu wa serikali ndizo hutumika.
Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa kipindi cha 2015-2016 ni shilingi Trilioni 22.5 na bajeti hiyo inatengenezewa mpango wa makusanyo na matumizi kwa kulipia mishahara ya wafanyakazi na miradi mbalimbali iliyoidhinishwa.
Pia katika matumizi mengine bajeti hiyo inalipia chakula cha wanafunzi, mikopo ya wanafunzi elimu ya juu, ununuzi wa dawa na vifaa tiba na chakula cha hifadhi ya taifa

0 comments:

-