Monday, November 23



KESI ya kuagwa kwa heshima kwa Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Geita, Marehemu Alphonce Mawazo, imefunguliwa katika mahakama kuu kanda ya Mwanza.

Kesi hiyo namba 10 ya mwaka 2015, imefunguliwa jana na familia ya marehemu Mawazo, imepangwa kusikilizwa kesho baada ya washitakiwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo na mwanasheria mkuu wa Serikali kupelekewa mashtaka.

Kesi hiyo inayosimamiwa na mawakili watatu, John Mallya, James Millya na Paul Kipeja, leo ilikuwa ni mara ya kwanza kusikilizwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, alidai kuwa kesi hiyo itatajwa leo baada ya washitakiwa hao kupelekewa samansi ya kesi inayowakabili.

“Tunashukru Jaji, Lameck Mlacha, amekubali kuisikiliza, kesi hii tuliofungua kwa hati ya dharura, katika mahakama ya kanda kuu ya Mwanza, kwani ni haki ya msingi kuagwa kwa mtu yeyote,” amesema Mallya.

Mallya alidai kuwa kesi hiyo imepelekwa mahakamani ili kuomba mahakama kutengua zuio la Polisi kuzuia kuagwa kwa mwili wa marehemu Mawazo, katika Jiji la Mwanza, Sengerema na baadae Geita.

Naye Wakiri, Paul Kapeja, ambaye pia ni Mbunge wa Simanjilo (Chadema), amesema kisheria polisi haina mamlaka ya kuzuia familia kuaga marehemu eneo lolote lile kwani ni haki ya kikatiba.

Kapeja alidai kuwa kitendo cha polisi kuzuia familia na kufunga barabara iliopo katika Ofisi za Chadema kanda ya ziwa Victoria ni kinyume na sheria na wanazuia waombolezaji kuaga mpendwa wao.

Mbowe awatuliza Wananchi
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewapongeza wananchi jijini Mwanza kwa kuguswa na tukio hilo la kinyama na kuwataka wawe na subira kwani suala hilo limefikishwa mahakamani.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, amesema wananchi wa Jiji la Mwanza wameonekana kuguswa na tukio hilo, kwani wamejitokeza kwa wingi mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

“Leo wakazi wa Mwanza tulikuwa pamoja na mmejitokeza kwa wingi kutuunga mkono, hali ambayo inaonesha namna gani mmeguswa na msiba huu, kesho mambo yatakuwa wazi,” amesema Mbowe.

Hali ilivyokuwa Mwanza
Jana wafuasi wa chama hicho na wananchi kutoka mahala mbalimbali walijitokeza mahakamani hapo kitendo ambacho kiliwanyima usingizi Polisi.

Umati mkubwa uliojitokeza leo mahakamani hapo, ulisababisha Polisi waliokuwa na silaha za moto, mabomu ya moto na machozi kuizunguka mahakama hiyo, huku kukitokea mvutano mkali uliotokana na Polisi kutaka wafuasi hao waondoke.

Hata hivyo katika vuta ni kuvute hiyo, mfuasi mmoja wa chama hicho ambaye hakufahamika jina lake alitiwa nguvuni na Polisi, ambako baadhi ya wapita njia katika eneo hilo kupata wakati mgumu wa kupita.

Pia gari la vikosi vya kutuliza ghasia (FFU) kutoka Tabora na Mara yalionekana jijini hapa, yakizunguka hali iliyotafsiriwa na wakazi wa jiji hili kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

0 comments:

-