Bushoke
Kama ulidhani Watanzania waishio nchini Afrika
Kusini wana kazi na maisha mazuri, basi ulikosea kwani kama huna elimu
ya kutosha ukaamua kuzamia nchini humo ni lazima utaishia katika mikono
isiyo salama.
Ruta Bushoke, ambaye alitamba na kibao
cha “Mume Bwege”, anasema maisha wanayoishi Watanzania wengi, hususan
wasanii, ni ya kusikitisha.
Akizungumza na Starehe
visiwani Zanzibar wakati wa tamasha la filamu la ZIFF, Bushoke alisema
wengi wao wanaishi kwa kutegemea biashara ndogondogo, ambazo hazina
faida kubwa huku wengi wao wakiishia kubebeshwa mizigo ya dawa za
kulevya na wafanyabiashara wakubwa kutoka nchi mbalimbali, hasa
Tanzania.
“Watanzania wengi wanajihusisha na biashara
za mihadarati, ile siyo nchi ya kwenda kichwa kichwa kwa sababu watu
wengine wana vyeti vizuri, lakini wamekosa kazi. Labda itokee bahati na
kule unakutana na mataifa ambayo huwezi kukutana nayo sehemu yoyote,”
anasema Bushoke.
Msanii huyo anasema wengi wanapenda
kuzamia bila kujua akifika kule atafanya shughuli gani, wengine
wanatamani maisha mazuri kwa kuyatazama juu juu lakini ni magumu.
“Kazi
wanazoweza kufanya wazamiaji ni kuuza vitu vidogovidogo kama simu,
samani au kitu chochote kilichoibwa, pia uuzaji wa dawa za kulevya kama
bangi,” anasema Bushoke.
Kwa mujibu wa Bushoke, wengi wanajishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya kwa kutuma watu na wengine wakisafirisha.
Akizungumzia
maisha yake nchini Afrika Kusini, Bushoke ambaye ni mtoto wa mtangazaji
Max Bushoke ambaye alikuwa nyota wa muziki wa dansi nchini, anasema
mipango yake ilikuwa kuishi kwa mwaka mmoja.
“Kule mimi
ni nyumbani, nilikuwa sijaenda kwa ajili ya kufanya kazi ila nilikwenda
kifamilia kwa kuwa wazazi wanaishi kule. Nilipanga kwenda kukaa mwaka
mmoja lakini nikajikuta nakaa miaka mitatu.”
“Sikupoteza
chochote kwa sababu baba yangu yupo kule na alizidi kunifundisha mambo
ya muziki kwa kuwa amenitangulia na anajua zaidi yangu. Kwa hiyo muda
mwingi tulikuwa tunaongea habari hizo na kunielewesha kuhusu muziki wa
kimataifa,” anasema Bushoke.
Hata hivyo, Bushoke
anasema akiwa nchini humo aliona fursa mbalimbali zinazohusu sanaa,
lakini kila alipojaribu hakufanikiwa ingawa kikubwa alichojifunza ni
kuhusu soko la kule na namna nafasi zinavyopatikana ili azitumie muda
mwafaka.
Anasema akiwa Afrika Kusini amefanya kazi mbalimbali za muziki ambazo ataziachia baada ya kupata usimamizi mwingine hapa nchini.
“
Baba yangu akienda kazini nilikuwa nabaki nyumbani kwa sababu mama
yangu anaishi Pretoria na baba Johannesburg. Kila siku nilibaki studio
ndogo pale nyumbani najifunza kupiga vyombo vya muziki mbalimbali,”
anasema.
Akizungumzia machafuko yaliyotokea Afrika
Kusini yaliyohusisha wenyeji kushambulia wageni kwa madai kuwa
wanawachukulia ajira zao, Bushoke anasema ingawa kipindi hicho hakuwa
nchini humo, amejifunza kuwa wazawa wamekuwa na dhana potofu kuhusu
wageni.
“Ni kitu ambacho sikishangai sana kwa Afrika
Kusini kwa sababu tunaishi nao tunawajua jinsi wanavyofikiria wao na
matatizo ambayo wameyapitia,” anasema.
“Tunapozungumza
nao wanatuambia wao walitawaliwa na wazungu, baada ya kupata uhuru
walitegemea kwamba mambo yangekuwa mazuri, lakini kumbe pamoja na uchumi
mkubwa wa nchi yao, vitu vingi bado wanavimiliki weupe.”
Anasema
kuwa kwa mtu wa kawaida, bado maisha yao ni ya chini kiuchumi na
yanaonekana yanazidi kuwa magumu kadri siku zinavyokwenda ndiyo maana
kunaibuka chuki dhidi ya wageni.
RSS Feed
Twitter
August 08, 2015
Unknown
0 comments:
Post a Comment