Tuesday, July 28

NIAJE maze! Ni Jumanne yenye kupendeza mbele za Mungu. Naamini wasomaji wangu wote mpo poa sana. Kama ndivyo, bado sifa ni za Mungu kwani kufika leo siyo uwezo wetu, ni yeye tu.
Baada ya wiki iliyopita kumaliza mada ya kila anayekutongoza ni lazima umwambie mumeo, leo niko na mada ya kati. Mada ya kati kwa maana kwamba, inasimama kotekote.
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu sana maisha ya wapendanao na kubaini yamejaa wivu, kisasi, chuki na kutoheshimiana.Mara zote, kila upande huwa unajitetea kwamba, upande mwingine haupo sahihi katika uhusiano ndiyo maana hakuna utulivu.

NAZUNGUMZIA MFANO HUU
Stela, ni mdada wa miaka 32, mkazi wa Kimara-Baruti, Dar. Alinipigia simu katikati ya wiki iliyopita na kuomba ushauri akisema mpenzi wake amekuwa na wivu sana siku hizi kiasi kwamba, hakuna furaha ya mapenzi tena kama zamani.
“Mfano nikitoka kazini, ananiuliza kama nimeshafika kwangu.

Hatukai wote. Nikimwambia bado, anakuja juu. Anasema nimepitia kwa wanaume ndiyo maana nimechelewa wakati si kweli. Yaani anko Ndauka imefika mahali naona kama ni mapenzi na yafe tu kuliko hii kero ya kila siku,” anasimulia dada Stela.
MASWALI YANGU KWAKE
Nilimuuliza Stela kama katika uhusiano wake na huyo jamaa amewahi kukutwa na tuhuma zozote za usatili? Maana amesema ‘…amekuwa na wivu sana siku hizi…’ hili neno siku hizi ndiyo nikawa nalitafutia kisa chake.
Stela akajibu: Kuna siku moja aliwahi kuona meseji ya jamaa mmoja tunafanya naye kazi alikuwa akinitongoza.
Swali: Ukamkubalia?

Jibu la Stela: Nilimkubalia ndiyo, lakini hatukuwahi kuduu. Jamaa yangu alipoiona hiyo meseji nikaona basi isiwe shida. Na yeye nilimwambia sitamkubalia na nikamuapia. Sasa kuanzia pale amekuwa na wivu wa kijinga sana.
HAPO NDIPO PENYE TATIZO
Nasema tatizo kubwa kwenye uhusiano ni usaliti. Mmoja kati ya wapenzi, akibaini usaliti mmoja tu, huondoa asilimia 90 ya uaminifu na kuingiza asilimia 100 ya kutoamini tena.Nimewahi kuwasikia wanawake wawili wakiwa baa, wakisema…
Mmoja:  Mimi mume wangu ameniruhusu kuingia kwenye siasa mwenzangu, wala hana neno na anajua kwenye siasa kuna wanaume kibao, lakini wala hana wivu.

Mwenzake: Wee! Mimi mume wangu hataki kusikia kitu hicho, yaani mume wangu hataki nifanye kazi yoyote ile inayohusiana na uwepo wa wanaume. Ana wivu kama nini!
HISTORIA NDIYO ZINA HUKUMU
Hawa wawili, ukiwafuatilia sana utabaini kuwa, huyu wa kwanza aliyeruhusiwa kujichanganya na wanaume hana simulizi yenye usaliti iliyowahi kumtokea ndani ya uhusiano, huyu wa pili, anayo. Lazima anayo.

Si mwanaume, si mwanaume. Kuongezeka  kwa wivu mara nyingi kunatokana na historia ya usaliti. Mmoja wa wapenzi anapobaini kasalitiwa, hata kama watakaa chini na kumaliza mambo, lakini nafasi ya kutomwamini mwenzake inaongezeka ukubwa kuliko awali. Fuatilia sana!
UTETEZI BILA KUSEMA UKWELI
Wapenzi walio wengi hupenda kusema ‘mwenzangu ana wivu sana’ bila kusema aliwahi kukumbwa na skendo gani ya usaliti siku za nyuma. Ikitokea wakasema na kuambiwa ndiyo sababu, hukimbilia kusema, ‘mbona ilikuwa zamani sana, tuliyaongea yakaisha’. Wanasahau kwamba, kwisha si hoja. Hoja ni ule moyo wa uaminifu kujeruhiwa. Tujiagalie hapo.
Tuonane wiki ijayo kwa mada nyingine.


0 comments:

-