Saturday, April 4


Katika  hali isiyo ya kawaida, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa na mbwa nane, waliweka doria katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika jana.
 
Ibada hiyo iliyoanza saa tisa jioni iliongozwa na Paroko wa Kanisa hilo, Audax Kaasa na Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo aliyetarajiwa kuiendesha kama ratiba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ilivyoeleza, lakini hakufanya hivyo bali alisali kama muumini wa kawaida. 
 
Gari ya polisi yenye namba PT 0964 iliegeshwa karibu na lango kuu la kuingilia kanisani humo, huku mbwa kadhaa wakizunguka katika maeneo mengine kuangalia usalama na baadaye waliingizwa katika gari hilo.
 
Haikujulikana sababu ya ulinzi huo katika kanisa hilo kwa kuwa makanisa mengine makubwa likiwemo Azania Front hakukuwa na hali hiyo.
 
Baadhi ya wadadisi wa mambo wanaihusisha hali hiyo na sakata linaloondelea kati ya Pengo na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, aliyemtolea maneno ya kuudhi hali iliyolilazimu Jeshi la Polisi nchini kuingilia kati.
 
Akitoa mahubiri, Paroko Kaasa alisema kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha waumini wa Kikristo kumrudia Mungu.
 
“Mungu anatutaka turarue mavazi yetu ili tumrudie, kipindi hiki tulipokuwa tukisikiliza historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo tumesikia namna alivyodharauliwa.
 
“Sijui katika maisha yako kama umewahi kukumbana na dharau aliyokumbana nayo Bwana Yesu, lakini yote hayo ameyaachia na kusema bwana uwasamehe kwa kuwa hawajui walitendalo,” alisema Paroko Kaasa.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema kipindi cha Kwaresma ni kipindi ambacho watu wanafundishwa uvumilivu na msamaha.
 
“Kipindi hiki watu tunafundishwa uvumilivu na msamaha, ni vyema kati ya dini na dini tukajifunza kuvumiliana na tukajifunza kutokutukanana.
 
“Kipindi hiki ni mwafaka kukumbushana uvumilivu kwa sababu dini zote duniani ndiyo nguzo ya amani na uadilifu, mafunzo yote yanayohusu amani na uadilifu ndiyo nguzo maalumu katika kudumisha amani ya nchi,” alisema Membe.
 
Katika hatua nyingine, alisema atatoa ufafanuzi leo kuhusiana na taarifa za kuwepo kwa vifo vya wanafunzi wa Watanzania waliokuwa wanasoma katika Chuo Kikuu cha Garissa cha nchini Kenya kilichoshambuliwa na kundi la Al Shabab na kuua watu 147.
 
Lowassa asali Ijumaa Kuu
Pia Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, amesema amani iliyopo nchini inapaswa kuenziwa kwa kuidumisha.
 
Kauli hiyo aliitoa baada ya ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, katika Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam jana.
 
“Tushukuru Mungu nchi yetu ina amani na Watanzania tuienzi amani kwa kuwa ndiyo imesaidia hadi leo tunasherehekea Ijumaa Kuu kwa pamoja. Tuitumie amani vizuri,” alisema Lowassa.
 
Naye, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, aliyekuwepo katika misa hiyo aliizungumzia Sikukuu ya Pasaka kuwa ni wakati wa kuonyeshana upendo.
 
“Tunaposherehekea tuwasaidie wenye upungufu na hilo ndilo jambo kubwa ambalo ni upendo mkubwa. Hii habari ya kusigana kwa namna yoyote katika dini zetu au wakulima na wafugaji isiwepo,” alisema Sumaye.
 
Katika ibaada hiyo Askofu Malasusa alilisihi taifa kuwa na unyenyekevu, utii na upendo kama aliouonyesha Yesu Kristo kwa wanadamu.
 
Naye, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, alisema kushamiri kwa vitendo vya kigaidi katika mataifa mbalimbali duniani kunatokana na watu kukosa moyo wa upendo.
 
Akizungumza jana wakati akiendesha ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza, alisema hali hiyo inatokana na kujengeka kwa chuki na uhasama ndani ya mioyo ya wanadamu katika miaka ya hivi karibuni.
 
Kwa upande wake, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Mchungaji Samweli Mshana, amesema hatua ya NEC kusogeza mbele upigaji wa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, kumewaondolea adha Watanzania kwa kuburuzwa na Serikali.
 
Akizungumza jana wakati alipohubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa la Usharika wa Dodoma mjini hapa alisema, kitendo kilichokusudiwa na Serikali ni kutaka kuwaburuza Watanzania wapige kura ya ndiyo kwa jambo ambalo hawalijui.
 
Alisema wapo Watanzania wengi wanaotakiwa kupata elimu ya kutosha juu ya Katiba Inayopendekezwa ili waweze kuwa na uhakika wa kile wanachokipigia kura tofauti na ilivyokuwa sasa.
 
“Tuna kila sababu ya kuipongeza NEC kwa uamuzi wa kuisogeza mbele kwa kuwa baadhi ya viongozi wa Serikali wasiokuwa na nia njema na taifa hili walitaka kutupeleka kama mifugo inayoenda kuchinjwa,” alisema Mchungaji Mshana.

0 comments:

-