Tuesday, March 31



Na Bashir Yakub
SUALA  la matunzo  ya  watoto/mtoto  limekuwa  ni suala  ambalo  wasomaji  wengi  wamekuwa  wakiniuliza sana. Wengi  wao  wanaouliza  ni  wale  ambao  wamezaa  nje  ya  ndoa  na  hivyo  kuna  utata  wa  matunzo  ya  watoto  na  wale  ambao  wamekuwa wanandoa  lakini  sasa  tayari  wametengana  aidha  kwa  talaka  au  bila  talaka.  Niseme  tu kwa  ufupi  kuwa  suala  la  matunzo  ya watoto  linajumuisha  mambo  mengi  nami  nitaeleza  baadhi  tu.
1. HUWEZI  KUMLAZIMISHA  MTOA  MATUNZO  KUTOA  AMBACHO  HANA
Kumekuwepo  na  tabia  ya  wazazi  hasa  upande  wa   wazazi  wa  kike   kuwalazimisha  wanaume  ambao  wamezaa  nao  na  kutengana  nao  kutoa  matunzo  ya  watoto  kwa  kiwango  cha  juu  kabisa  ambacho  pengine   kinazidi  hata  kipato  cha   mtoaji. Hili  si  sawa. 
Ni  kweli sheria  inamlazimisha  mwanamme  kutoa  matunzo  ya  mtoto    lakini  haimlazimishi  kutoa  kuliko  anachopata. Sheria   haisemi  kwa kuwa  mwanamke  anaishi  na  mtoto  wa  mtu  basi mwanamme   ndiyo  sasa afanywe  kitegauchumi.  Inafikia  hatua  mwanamke  hafanyi  kazi  yoyote  isipokuwa  anategemea  ile  pesa  ya matunzo  ya  mtoto  ndiyo  iwe  kila  kitu  katika  maisha  yake.
Hii  ndiyo  sababu  hata  akipewa  kiasi   kinachotosha  haoni  kama  kinatosha  kwa kuwa kinakuwa  na  njia  nyingi  kama  saluni, nguo za kuvaa,  pesa  ya  upatu, michango  ya  harusi  na  ‘kitchen  party’  na  kila  kitu  kinachohusu  maisha  yake binafsi.  

Ieleweke  wazi  kuwa  kwa  mujibu  wa  sheria,  pesa  ya  matunzo  ya  mtoto  haihusiki  na  haya.  Pesa  ya  matunzo  ya  mtoto  ni  pesa  ya  matunzo   ya  mtoto  kama   neno  lenyewe  lilivyo  na  linavyojieleza si  vinginevyo.
2. INARUHUSIWA  KUKATAA KULAZIMISHWA  KUTOA  MATUNZO YANAYOZIDI  UWEZO
Ikiwa  mwanamme  analazimishwa  kutoa  kuliko  kipato  chake  basi  anaruhusiwa  kukataa  hata  kama  amri  hiyo  imetolewa  na  mahakama. Wengine  huandikishana  polisi  lakini  bado  haibadili  maana  kwa kuwa  mtu  anatakiwa  kutoa  kulingana  na  uwezo wake  au  kipato  chake.
Wapo  wazazi  hasa  wa kike   ambao  huwalazimisha  wanaume  kutoa  matunzo ya  kuwasomesha  watoto   katika shule za kimataifa zenye kutumia lugha za kigeni (international  schools)  wakati  kipato  cha  mwanmme  ni  shule  ya  kata.
Sheria  inachokataza  ni  kukataa  kabisa   kutoa matunzo  ya  mtoto  lakini  haimlazimishi  mtu  kutoa  kilichomzidi.  Au  wengine  hulazimisha  kuwekewa  mpaka  wafanyakazi  wa  ndani (house girls)  wakati  kipato  cha  mwanamme   hakiruhusu  jambo  hilo.
Huu  nao  ni  unyanyasaji  kwa  upande  wa  wanaume  na  haukubaliwi  na  sheria.  La  msingi  ni   kuwa  iwapo  utalazimishwa  kutoa  kuliko  uwezo  wako   wewe  kataa.  Na  kama  uamuzi  huo  umetolewa  na  mahakama  basi kataa  kwa  kukata  rufaa  kupinga  kabisa  jambo  hilo.
Sheria  inaposema  matunzo  ya  watoto  haisemi  kuwa  watu  watoe  kuliko uwezo  wao  hapana. Sheria  ni  haki   na  haki  huzingatia  ukweli  na  hali  halisi  ya  jambo.
3. UMRI  WA  WATOTO  KUISHI  NA  MAMA  AU  BABA
Mara  nyingi  sheria  imeelekeza  watoto  walio  chini  ya  umri  wa  miaka  kumi    yaani  kuanzia  miaka  tisa  kushuka  chini  kuishi  na  mama.  Aidha  kuanzia  miaka  kumi  kwenda  mbele  mtoto  anaweza  kuchagua  aishi  na  nani  kati  ya  baba  au  mama. 
Kwa hiyo  iwapo  mtoto  amefikisha  umri  wa  miaka  kumi  au  zaidi  basi    baba  anaweza  kumchukua  mtoto  wake,  iwapo  pia  mtoto  atapenda  kukaa  na  baba  yake. Wapo wazazi  ambao  wamekuwa  wakiwanga’nga’nia  watoto  hata  baada  ya watoto  kuvuka  umri  huo  ili  waendelee  kuwafanya  vitega uchumi  kupitia  kudai  matunzo. Hili  si  sawa   hasa  iwapo  mtoto  yuko  tayari  kukaa  na  baba.
4. BABA  ANAWEZA  KUOMBA  KUKAA  NA  WATOTO  HATA  KAMA  NI  WADOGO
Hapo  juu  tumeona  kuwa  ni  lazima  mtoto  kukaa  na  mama  iwapo  ana  umri  chini  ya  miaka  kumi.  Msimamo  huu  unaweza  kubadilika  iwapo  baba  atatoa  sababu  za    msingi  za  kuomba  mama  asikae  na watoto.
Hii  haijalishi  watoto  wana  umri  gani   iwapo  tu ana sababu  za  msingi  basi  ataomba  kukaa  na  watoto/mtoto  wake.  Sababu  kubwa  za  kuomba  watoto  ni  iwapo  mama  ana  ugonjwa  wa  akili  na  hivyo  kuwa  hatari  kwa  ustawi  wa mtoto/watoto.
Pia  iwapo  mama  anakaa  na  watoto  katika  mazingira  hatarishi  kama  danguro, baa, sehemu  za  madisco, au  mama  anajihusisha  na  vitendo  vya  ukahaba  ambavyo  si  vyema  kabisa kwa  makuzi  ya  mtoto.
Hii  inajumuisha  matendo  yote  maovu  ambayo   kukaa  na  watoto/mtoto   yanaweza  kuleta  athari  mbaya  kwake  na  ni hapo   baba  atakapoomba  kuchukua  mtoto/watoto  na  atakubaliwa  bila  kujali  umri  wa  watoto.
5. HAKI   YA  KWENDA  KUWAONA  WATOTO
Wapo  watu  ambao  huzuiwa  kuwaona  watoto. Wengine  huruhusiwa  lakini  kwa  masharti  maalum  na  kwa  kupewa  muda  wa  kuzungumza nao. Hii haikubaliki,  kisheria  mzazi  anapaswa  kuwaona  watoto  kwa uhuru  na bila  masharti  yanayolenga  kumwondolea  haki  hiyo.
Ikiwa  mzazi  anazuiwa  kuwaona  watoto/mtoto  au  anawekewa  masharti  magumu  basi  anaweza kudai  haki  hii  kwa  kupeleka  malalamiko  ustawi  wa jamiii au  mahakamani    haraka  iwezekanavyo.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   ‘HABARI   LEO’  KILA  JUMANNE,  GAZETI  ‘JAMHURI’   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  ‘NIPASHE’  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com.   KUPATA  USHAURI   WA  SHERIA  ZA  ARDHI, NDOA, MIRATHI, MAKAMPUNI,’

0 comments:

-