Monday, October 13

MFANYAKAZI wa kujitolea ambaye alitumia Paundi 5,000 (sawa na Sh 12,500,000 za Tanzania) kumleta mkewe mpya kutoka Jamaica hadi Uingereza amejikuta akiumizwa moyo baada ya mke huyo kumuacha dakika 20 tu baada ya kufika nyumbani kwa mumewe.

Johnny Gannon alitumia maelfu ya fedha kumtafutia Visa Patrice Chambers (24) ili waweze kuishi kama mke na mume katika nyumba yake iliyopo Perth, Scotland, lakini mara tu baada ya Patrice kuwasili Perth, alimtuma Gannon (57), kwenda kununua chakula.

Hata hivyo aliporudi msichana huyo alinyakua mabegi yake na kumwambia anaondoka. Dakika 20 baada ya kuwasili nyumbani kwao, msichana huyo alikimbilia kwenye gari na kisha kupanda treni na kutokomea.

Mumewe amegundua pia Patrice amemwachia bili ya paundi 500 ( sawa ni Sh 1, 250,000)katika simu yake ya mkononi.

Gannon aliyeumizwa moyo, alifunga ndoa na Patrice mjini Jamaica mapema mwaka huu, akiamini mkewe mpya amekimbilia Bristol kukutana na mpenzi wake ambaye ni Mjamaica ambaye walichonga mpango wa kutoroshana.

Alilieleza gazeti la Daily Mirror, “ nilikuwa na matarajio makubwa ya kuishi maisha yangu yote na Patrice , lakini nadhani alikuwa ameshaweka mipango yake ya kufanya hili… uhusiano wangu na yeye sio wa kuonana kwenye baruapepe. Nimemfahamu kwa miaka miwili na alionekana kuwa mkweli kwangu. Amenitumia na najisikia kudhalilishwa.

Nilikuwa na maono ya furaha mbele yetu. Najiona mjinga.” Gannon alikuwa akienda mara kwa mara Jamaica kwa ajili ya mapumziko na ndipo alipokutana na Patrice miaka mitatu iliyopita. Rafiki aliwakutanisha, pamoja na utofauti wa miaka 33 alimpenda mara baada ya kukutana kwa mara ya kwanza katika baa ya hoteli iliyopo Treasure Beach.

“Alikuwa akiendesha baa ndogo na nilikuwa nikikaa naye pale. Ni msichana mwerevu na mimi nilifikiri ni patna anayestahili katika maisha yangu.”

“Ni kweli nilikuwa nikijifinya mara nyingine maana nilikuwa siamini jinsi nilivyokuwa na bahati kupata mwanamke kijana mzuri. Lakini uhusiano wetu ulikuwa ukiendelea vizuri kila muda ulivyokuwa ukienda vizuri, kwa hiyo sikutegemea kuumizwa kwa kiasi hiki,” alisema.

Alisikia kutoka kwa rafiki wa Patrice kuwa binti huyo alikuwa na rafiki wa kiume Uingereza lakini alipomuuliza alijitetea kuwa alikuwa ni jamaa wake wa zamani.

Mapenzi aliyokuwa nayo kwa msichana huyo yalimfanya amuamini na aliendelea kuonana naye kila alipokuwa akienda Jamaica. Gannon anasema Patrice ndio alianza kugusia habari za kufunga ndoa na sherehe iliandaliwa katika safari yake moja alipokwenda Jamaica.

Alilipia gauni la bibi harusi na hela ya kutengenezea nywele kwa ajili ya siku ya harusi na aliporudi Scotland alianza kushughulikia viza kwa ajili ya msichana huyo. Mwisho Gannon alimtumia Patrice paundi 700(1,750,000) kwa ajili ya kushughulikia makaratasi nchini Jamaica na alimtumia fedha zaidi baada ya kudai kaibiwa. Mwaka huu pekee Gannon ametumia zaidi ya Paundi 4,000 (sawa na Sh 10,000,000 za Tanzania) kwa ajili ya Patrice.

Marafiki waliwapokea Gannon na mkewe walipowasili kwa ndege katika uwanja wa Edinburgh kwa ajili ya kwenda kuanza maisha yao mapya kama mke na mume lakini Patrice alimwambia hataki kuishi naye na Gannon aliporudi kutoka kufanya manunuzi kwa ajili ya mkewe alimpeleka kwenye stesheni ya treni.

Gannon ametoa taarifa Polisi na amepanga kuwasiliana na Wakala wa Uhamiaji Uingereza na anafikiria atamwambiaje mama yake kuhusiana na fedheha hiyo.

0 comments:

-