Monday, August 11

Picha no 1
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Siku ya Vijana Duniani itafanyika tarehe 12 Agosti, 2014 ikiwa na lengo la kuyafanya masuala mbalimbali ya vijana kutambulika katika jamii ya Kimataifa. Mwaka huu, ujumbe ni “Vijana na Afya Kiakili”.  Tarehe hii iliamuliwa kuwa Siku ya Vijana Duniani na Umoja wa Mataifa mwaka 1999. Hii ni Siku maalum inayodhihirisha kutambua kazi muhimu zinazofanywa na vijana na umuhimu wake katika jamii pamoja na kuwapa fursa kwa ajili ya kuongeza ufahamu juu ya changamoto na matatizo yanayoukabili ulimwengu wa vijana.Mijadala katika maeneo maalum pamoja na taarifa juu ya kampeni mbalimbali zitafanyika katika maeneo na nchi mbalimbali ulimwenguni kwa ajili ya kutoa hamasa kwa nchi wanachama pamoja na jamii ili kuelewa mahitaji ya vijana, utekelzaji wa sera mbalimbali katika kusaidia kupambana na changamoto zilizopo, pamoja na kuwasaidia vijana kushiriki katika michakato ya utoaji wa maamuzi.

Siku ya Vijana Duniani ni kutambua na kuthamini kuwa kipindi cha ujana kinaambatana na mabadiliko makubwa na ya haraka na safari ya kutoka utotoni kufikia utu uzima inaweza kuwa ngumu na yenye changamoto nyingi na hivyo kuhitaji utulivu na ukomavu wa akili. Kwa Tanzania kijana ni mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.
Katika Siku hii na siku za mbeleni itakuwa fursa ya kuweza kutoa ufahamu juu vikwazo mbalimbali vinavyowakabili vijana ikiwemo kunyanyapaliwa na kubaguliwa, lakini pia kuwapa vijana nguvu ili waweze kutimiza malengo yao.
Tanzania kama sehemu ya duania inatambua na kuthamini changamoto maalum zinazowakabili vijana walioko katika mazingira hatarishi pamoja na umuhimu wa kuhakikisha kuwa wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya maendeleo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na vijana pamoja na wadau wa maendeleo ili kuunga mkono programu za elimu ya afya kwa vijana walioko ndani na nje ya shule, walioko katika taasisi za mafunzo rasmi na zisizo rasmi ili kukuza uwezo wa taarifa na mawasiliano ya kisasa.
Katika ngazi ya kitaifa Tanzania imedhamiria kukuza na kuboresha misingi ya kuwashirikisha vijana katika maeneo ya sera mbalimbali, programu ya mikakati ya maendeleo ya vijana ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika na kufanyiwa kazi.
Katika kutekeleza eneo hili Tanzania inalenga kuweka fursa zitakazowawezesha vijana kukuza utaalamu na ujuzi utakaowawezesha kufanikiwa katika kipindi cha mpito kutoka ujana kwenda katika utu uzima kwa kuzingatia hali halisi ya mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani.
Kwa kutambua umuhimu huu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inatumia fursa hii kuwakaribisha vjana pamoja na wadau mbalimbali katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa ya mwaka huu ambayo yatafanyika Mkoani Tabora kuanzia tarehe 08 – 14 Oktoba ikiwa ni mwedelezo wa kuwapa vijana na wadau taarifa mbalimbali kuhusiana na maendeleo kwa ujumla wake.
Tukiwa tunasherehekea Siku ya Vijana Duniani Wajibu wetu mkubwa ni kuona kuwa vijana wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jamii wanazoishi.
Katika Siku hii Vijana wote wanakaribishwa kuandaa hadithi mbalimbali fupi zenye mafunzo, mashairi, picha mbalimbali, video na kazi za sanaa ili kazi itakayoonekana inafaa iweze kuwa miongoni mwa kazi zitakazojumuishwa katika Chapisho la Umoja wa Mataifa ‘Kuwajumuisha Vijana Kijamii kwa kuzingatia Afya Kiakili’.
Imetolewa na wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo

0 comments:

-