Sunday, August 3


Mitandao ya kihalifu inazidi kujiimarisha nchini na sasa kumeibuka makundi ya wauaji wa kukodi katika mikoa ya kaskazini mwa nchi pamoja na Kanda ya Ziwa.
Mbali na mauaji ya albino na vikongwe ambayo yalipata kutikisa katika maeneo kadhaa ya nchi, wauaji wa kukodi wanatumika kutekeleza uhalifu huo kwa lengo la kulipiza kisasi, uporaji wa fedha, kujitanua kibiashara au kudhulumu mali na fedha.
Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na gazeti la mwananchi umebaini kuwa silaha nyingi zinazotumika katika mauaji ya kukodi yanayofanyika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, hununuliwa ama kukodishwa kutoka Namanga upande wa Kenya.
Wauzaji wa silaha hizo ni ama raia wa Kenya wenye asili ya Kisomali ama wahamiaji haramu wenye asili ya Kisomali wanaoingia nchini, wakitokea Somalia kupitia Kenya.
Uchunguzi umebaini kuwa bunduki aina ya Submachine Gun (SMG) huuzwa kati ya Sh3 milioni hadi Sh5 milioni na bastola zikiuzwa kati ya Sh500,000 na Sh1.2 milioni.
Pamoja na kutoka nje ya nchi, wauaji wengine wa kukodi hupatikana nchini kulingana na aina ya mtu wa kuuawa, mazingira na ugumu wa kazi.
Kwa Tanzania, mikoa inayoongoza kwa kuwa na wauaji wa kukodi ni Arusha na Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukiguswa kuwa jirani na mikoa hiyo.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mtoa taarifa wetu alisema alisema: “Hata sasa ukihitaji vijana wa kazi nitakuunganisha. Jambo muhimu hakikisha huwarushi (unawapa fedha zao), ukiwarusha lazima na wewe watakuua.”
“Yupo rafiki yangu anayewafahamu vyema kwa sababu amewahi kuwaunganisha na waliokuwa wakihitaji huduma yao,” alisema mtoa habari huyo.
Malipo ya kuua
“Malipo kwa kazi hii yanaanzia kati ya Sh1 milioni na Sh5 milioni kutegemea na uzito wa kazi husika,” alisema mtoa taarifa wetu anayeishi Arusha na akithibitisha kwamba anafahamiana na madalali wa wauaji hao.
Alisema mara nyingi wauaji hao hawataki kukutana na wateja moja kwa moja ili kuepuka kutambulika, badala yake hukutana au kuwasiliana na mtu wa kati (wakala) ambaye pia hupokea malipo na kuwakabidhi.
Hata  hivyo, uchunguzi  ulibaini kuwa kiasi cha malipo kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ni kikubwa ikilinganishwa na Kanda ya Ziwa ambako hulipwa fedha kidogo.
Vyanzo hivyo vimedokeza malipo wanayopata katika mikoa hiyo ni Kati ya Sh200,000 hadi Sh1 milioni kwa kuzingatia eneo husika na walikotolewa na kwamba fedha hizo huwa ni ujira wa watu wawili au zaidi.
Katibu wa Jumuiya ya Kuhifadhi Mila na Desturi za Mtanzania Kanda ya Ziwa, Gambang’adi Kaliba anasema wanaokodiwa ni wale wasiokuwa na vipato, walevi na wavuta bangi ambao wamekata tamaa ya maisha, hivyo hupewa fedha kidogo kwa ajili ya mauaji hayo ya kikatili.
“Watu wanalipwa Sh200,000 mpaka 500,000 kwa kuwa hawafanyi kazi wanaziona nyingi na wamekuwa wakijulikana katika baadhi ya maeneo kwa kuwa wakilewa hutamba na kuwa wako tayari kumwaga damu ya mtu maadam wapewe fedha,” anasema Kaliba.
Mkoani Mara, uchunguzi ulibaini kuwa kumekuwapo na mauaji ya aina hiyo na kwamba malipo kwa kifo cha mtu huwa ni kati ya Sh300,000 na 500,000.
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu wilayani Ukerewe ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe anasema wanapowakamata wahusika wa mauaji, baadhi hukiri kukodiwa kwa malipo ya Sh200,000 na kwamba idadi yao huwa ni kati ya watu wawili au watatu.
Mifano hai
Chanzo kimoja kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Manyara kilisema kuwa mauaji ya mmoja wa wafanyabiashara yalifanywa kwa kutumia mtandao huo.
Aliuawa mwaka jana wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
“Mirerani ndiyo umafia huo unatumika sana unajua kule ni unyama unyama kwa hiyo mtu kukuua kwa sababu ya mawe ni jambo la kawaida,” alidokeza polisi huyo.
Habari za kipolisi zinaeleza kuwa wauaji wa mfanyabiashara huyo walilipwa kati ya Sh3 milioni milioni na Sh5 milioni baada ya kukodiwa mahususi kutekeleza mauaji hayo.
Bunduki aina ya SMG inayodaiwa kutumika katika mauaji hayo ilinunuliwa kwa Sh4 milioni katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga kutoka kwa watu wenye asili ya Somalia.
Mauaji mengine yanayofanana na hayo yalitokea Januari 26, 2006 saa 2:30 usiku nje ya klabu maarufu ya Peters Club iliyopo Majengo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Siku hiyo watu waliokuwa na SMG walimmiminia risasi mfanyabiashara wa magari ya ‘dili’, Aristarik Msacky (34) na kutochukua chochote isipokuwa simu yake ya mkononi.
Kabla ya kuuawa, mfanyabiashara huyo alikuwa akinywa pombe na marafiki zake ndipo alipopigiwa simu ili atoke nje kuna ‘biashara’ na alipotoka nje ya baa ili kukutana nao ndipo alipouawa.
Tukio jingine ni lile la mkazi wa Kijiji cha Nyichoka wilayani Serengeti, Mara ambaye alituhumiwa kumuua mwendesha pikipiki (bodaboda), Julai 5 mwaka huu ambaye kwa mujibu wa polisi, alikiri kufanya mauaji hayo kwa kukodiwa.
Polisi walisema mtuhumiwa huyo (jina tunalihifadhi) alikiri kwamba yeye na mwenzake ambaye aliuawa  na wananchi wenye hasira kali, walikodiwa na mkazi wa Park Nyigoti kutekeleza mauaji hayo kwa Sh500,000 kwa madai kuwa bodaboda alikuwa na uhusiano na wake zake.
Hata hivyo, mpaka wanatekeleza mauaji hayo kwa kumkatakata na kumtumbukiza mtoni, walikuwa wamelipwa Sh40,000 tu na kati ya fedha hizo Sh20,000 zilikuwa za kukodi pikipiki na zilizobaki kwa ajili ya chakula. Hadi mmoja alipouawa na yeye kukamatwa walikuwa wakimdadisi ‘bosi’ wao Sh460,000.
Msemaji wa Polisi
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema polisi wapo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao na hivyo ndivyo wamekuwa wakifanya kila wakati, kutimiza wajibu huo.
Senso alisema kwamba endapo wakibaini kuwa kuna watu wanafanya uhalifu wa namna hiyo huwakatama na kuwafikisha mahakamani, huku akitoa mwito kwa wananchi na jamii nzima kutimiza wajibu wao wa kutoa taarifa za makundi kama hayo katika maeneo wanayoishi.
via>>Mwananchi

0 comments:

-