Wakati wanawake
kwa wanaume wengi huenda barani Asia, hasa China kununua bidhaa kwa
ajili ya kuja kuzichuuza, hali sasa ni tofauti kwa kuwa kuna wasichana
ambao huenda huko kwa ahadi za ajira, lakini huishia kufanya ukahaba
kwenye madanguro, gazeti hili linaweza kukuthibitishia.
Wasichana hao hutafutwa na mawakala wa hapa nchini
ambao kazi yao huwa ni kutafuta wasichana wazuri na baadaye
kuwashawishi kwa kuwaeleza fursa za ajira za hotelini zilizo barani
Asia.
Msichana akikubali, wakala huchukua jukumu la
kumtafutia viza ya kuingia China na baadaye kuwasiliana na mwenyeji
wake, maarufu kama Lady Boss, ambaye hutuma tiketi ya ndege kwa ajili ya
kumsafirisha ‘mwajiriwa’ mpya.
Hata hivyo, hali hubadilika mara wafikapo huko kwa
kuwa ‘mwajiri’ huyo humpokonya hati ya kusafiria na baadaye kumpa
maelekezo kuwa atatakiwa kulipa Dola 200 kila siku ambazo atakuwa
akizipata kwa kufanya umalaya kwenye klabu na maeneo ya biashara.
Tayari wasichana kadhaa wa Kitanzania wamenaswa
katika mtego huo na kujikuta wakilazimika kuuza miili yao ili wamudu ada
ya Dola 200 pamoja na fedha za kujikimu, akiwemo Munira Mathias mwenye
umri wa miaka 23 ambaye alimudu kuvaa ujasiri wa kuweka bayana uovu huo
katika mazungumzo yake na gazeti hili.
Binti huyo Mtanzania aliyesafiri kwa saa 18 kwenda
Guangzou, China alitakiwa kupumzika kwa saa mbili tu kabla ya kupelekwa
kuanza ‘kazi’ ambayo hakuitarajia.
“Baada ya kupumzika kwa saa mbili tu, nilipelekwa kwenye klabu,” anasema Munira wakati akisimulia mkasa wake.
“Sikuwa na kazi nyingine zaidi ya kucheza muziki
na wanaume ambao licha ya kwamba sikuwahi kuwaona, walinichangamkia kama
vile wananifahamu.”
Munira aliondoka Januari mwaka huu kwenda China
ambako aliahidiwa kuwa angeajiriwa hotelini, lakini alikutana na ‘ajira’
ya ukahaba, huku akilazimika kuwalipa ‘waajiri’ wake Dola za Marekani
200 kila siku.
Binti huyo, ambaye alifanikiwa kuchomoka mikononi
mwa waajiri hao baada ya viza yake kuisha, alisema kwa siku 91 alizokaa
China, alipata mateso ambayo hatayasahau ikiwamo kupigwa, kubakwa na
kundi la wanaume raia wa Nigeria, pia kulazimika kutoa mimba aliyoipata
kwa kubakwa.
“Nilifika Guangzhou kama saa 9.00 alasiri za
China na kulikuwa na baridi sana,” anasema Munira akisimulia jinsi
alivyokanyaga kwa mara ya kwanza ardhi ya nchi hiyo akiwa na matumaini
ya kuanza maisha mapya.
“Wakati huo nilikuwa nikijaribu kupata mawasiliano na mwenyeji wangu ambaye niliagizwa kutoka Magomeni, Dar es Salaam.Alisema alipotoka Dar es Salaam aliambiwa angepokewa na mtu
anayeitwa Jacky ambaye hakumkuta kwa kuwa alikuwa safarini Malaysia,
lakini alikuwa ameacha maagizo apokewe na mwanamke mwingine.
“Nilielekezwa nikodi taksi hadi kwenye hoteli
inayoitwa Nairobian. Kutoka hapo uwanja wa ndege hadi kwenye hiyo
hoteli ni sawa na umbali wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es
Salaam hadi Bagamoyo,” anasema Munira.
Anasema alitakiwa kulipa Yuan 200 (Sh60,000) na alipofika katika hoteli hiyo alipokewa, akaoga na kupewa chakula.
“Nilipomaliza kula nilipumzika kwa saa mbili
hivi. Jacky alikuwa amesharudi na alinifuata chumbani na kuniambia
natakiwa kwenda saluni. Hivyo tuliondoka pamoja hadi kwenye jengo kubwa
lenye maduka makubwa linaloitwa Tin- shu,” anasimulia Munira.
Watanzania lukuki
Katika jengo hilo alishangaa kuwaona Watanzania
wengi, wakiwamo wanawake kadhaa ambao aliwahi kukutana nao Magomeni
wakati akifuatilia safari yake.
Munira anasema miongoni mwa watu aliowaona ni binti mmoja ambaye wanafahamiana ambaye alistaajabu kumwona sehemu hiyo.
“Aliniuliza kwa mshangao, ‘mbona umekuja huku?
Umekuja kufanya nini?’ Wakaanza kunishangaa. Yule msichana akaniambia
‘huku msala ndugu yangu, umekuja kufanya nini?” alimnukuu na kuongeza
kuwa kabla hawajamaliza mazungumzo yao, mwenyeji wake alitokea hivyo
waliyakatisha.
Anasema waliingia saluni ambako aliwakuta
Watanzania na Wakenya wakifanya kazi humo na wakati yeye akiendelea
kusukwa nywele kwa umaridadi, Jacky alikwenda kumnunulia nguo na viatu
dukani.
“Baada ya hapo niliambiwa nivae nguo niende klabu
kwa sababu huo ni msimu wa sikukuu za mwaka mpya wa Kichina,” alisema
Munira.
Anasema alishangaa kuambiwa aende klabu usiku huo wakati alikuwa amechoka kwa safari ndefu.
“Kilichokuwa kinanipa moyo usiku ule ni kuwa
niliwaona wasichana wa Magomeni, lakini nilihisi wameambiwa wasiwe
karibu na mimi.”
Anasema alipoingia klabu, pia alishangaa zaidi kukutana na
Watanzania wengi wa rika tofauti ambao baadhi yao aliwatambua kwa sura
na pia kulikuwa na raia wengi wa Nigeria.
“Kiasi fulani nilifarijika kuwaona Watanzania na
nilijisikia kukua kiakili baada ya kuwaona Wanigeria ambao nilizoea
kuwaona kwenye filamu peke yake,” anasema.
Hata hivyo, alishangaa kuona pale klabu
alichangamkiwa na watu wengi, lakini hakutaka kudadisi zaidi bali
alidhani ndiyo hali halisi au alikuwa na bahati ya kupendwa.
“Baada ya kumaliza kucheza muziki kwenye klabu hiyo, walipelekwa kwenye klabu nyingine ya asubuhi.
“Tuliporudi hotelini, nilijitupa kitandani na
kulala kwa sababu ya uchovu mwingi. Miguu ilikuwa imevimba kwa sababu
nilikuwa nimevalishwa viatu virefu na kucheza muziki mfululizo. Nikalala
bila ya hata kuoga,” anasema.
Mwanzo wa mateso
Baada ya saa moja kupita na akiwa amelala fofofo mchana ule, mara aliamshwa na Jacky, ambaye alimwamuru amkabidhi pasipoti yake.
“Nikampa, pasipoti yangu nilikuwa
nimeiambatanisha na tiketi na kila kitu. Akanishangaza kuniambia kuwa
kuanzia siku hiyo niwe nampelekea Dola 200 mezani kila siku. Nilishangaa
na nikaanza kulia,” anasema.
Kwa hasira na mshtuko alioupata, Munira anasema
alitoka nje na kuanza kulia na wenzake walipomuuliza kinachomliza,
aliwaeleza. Waliamua kumwambia ukweli kwamba hata wao walipelekwa kwa
miadi ya kupata ajira za hoteli, lakini hawafanyi hivyo.
“Waliniambia kuwa nao walirubuniwa na
wakanyang’anywa hati za kusafiria kama mimi na wakaishia kuambiwa
wafanye biashara ya kuuza miili ili watafute fedha,” anasema Munira.
Munira anasema alichanganyikiwa, hasa pale
alipoambiwa na wenzake kwamba kazi kubwa ni kwenda klabu kujiuza au
kuzurura eneo la Chambu Chambu.
Chambu Chambu ni soko la bidhaa ambako wasichana
hujifanya wananunua vitu, lakini kimsingi huwa wanakwenda kutafuta
wateja wa ngono.
“Kule wanaume wameshajijengea picha kuwa wanawake wa Kitanzania
wapo kwa ajili ya kujiuza, basi wakikuona tu wanakufuata na mnaongea
biashara, mnakwenda kumalizana,” anasimulia.
Wasichana wenzake wa Kitanzania walimwambia kuwa
hayo ndiyo maisha yenyewe, hivyo aliporejea ndani, mwenyeji wake (Jacky)
alimwambia ajiandae kuanza kazi mara moja na Munira akawa hana budi
kufuata maelekezo.
Baada ya hapo aliingia bafuni akaoga, kisha akaenda eneo la Chambu Chambu kutafuta wateja.
“Nikakubaliana na hali halisi nikawa nafanya
kazi kama nilivyoambiwa. Niliona nikubali lakini akili kichwani mwangu
ilikuwa nifanye mbinu ili nirudi nyumbani,” anasema.
Simulizi ya Munira itaendelea kesho kwenye kijarida cha Ndani ya Habari.
* Munira Mathias si jina halisi-Mhariri
0 comments:
Post a Comment