Sunday, April 6




Marehemu Edna Sangawe (34) enzi za uhai wake.
My God! Bibi harusi mtarajiwa aliyejulikana kwa jina la Edna Sangawe (34), mkazi wa Mikocheni B jijini Dar anadaiwa kunyongwa na watu wasiojulikana na mwili wake kutelekezwa maeneo ya Changanyikeni, Makongo-Juu, Dar, Risasi Jumamosi lina kisa kizima.ILIVYOKUWA

Kwa mujibu wa chanzo makini, Machi 31, mwaka huu muda wa saa 2:00 usiku, bwana harusi mtarajiwa aliyetajwa kwa jina moja la Stanley, alipigiwa simu na mtu asiyemjua kuwa aende mbali kidogo na kwake.

“Aliyempigia simu alimwambia anamhitaji kwa ajili ya matengenezo ya friji kwani Stanley ni fundi wa mafriji.

“Bila kujua kinachoendelea, jamaa alikwenda hadi mahali alipoelekezwa na aliambiwa akifika mahali hapo asigonge geti mpaka mtu huyo atakapofika, alipofika hakuona mtu na alipopiga simu haikupokelewa,” kilisema chanzo hicho.

Ilielezwa kwamba, kwa kuwa hakukuwa na dalili za mtu yeyote kuonesha kumuita, Stanley aliamua kurudi kwake, alipofika hakumkuta mchumba wake ambaye alimuacha anapika.

APATA SHAKA

Ilifahamika kwamba jamaa huyo alipoingia ndani kwake alijaribu kumtafuta Edna bila mafanikio ndipo akahisi huenda atakuwa amekwenda kafuata mahitaji dukani lakini muda ulizidi kuyoyoma, alimua kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu (Mlimani) ambapo polisi walimwambia zikipita saa 24 arudi tena.




Marehemu Edna Sangawe.
AKUTWA AMENYONGWA

Ilizidi kudaiwa kwamba katika kuendelea kumtafuta kwa kuulizia nyumba hadi nyumba ndipo jirani mmoja alipomwambia kuwa alisikia kelele kwa mbali na waliposogelea eneo alilosikia sauti walimkuta Edna akiwa amenyongwa.

Stanley alirudi Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu na kutoa taarifa ambapo polisi wafika eneo la tukio na kuchukua mwili huo na kuupeleka katika Hospital ya Taifa Muhimbili, Dar kwa uchunguzi zaidi. 

POLISI WAMSHIKILIA MCHUMBA’KE

Ilifahamika kwamba ilibidi polisi wamshikilie Stanley kwa uchunguzi zaidi na pia kwa usalama wa maisha yake kwa kuwa siku ya tukio, Stanley ndiye aliyekuwa pamoja na marehemu.

MAJIRANI WA MAREHEMU WASHTUKA

Wakizungumza na gazeti hili huku wakiomba kutotajwa gazetini, majirani wa marehemu walisema walipokea taarifa hizo kwa mshtuko kwani awali walidhani ni utani wa Sikukuu ya Wajinga (Aprili Mosi).

“Mwanzoni tulijua ni utani kutokana na leo ni siku ya wajinga lakini niliwashauri wenzangu tuelekee Kituo cha Polisi cha Chuo Kikuu kufahamu baada ya kupigiwa simu na mmoja wa wanandugu wa mwanaume, tulipofika kituoni ndipo tukaamini,” alisema mmoja wa majirani hao.

 
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Dar, ACP Camillus Wambura.
KABLA YA TUKIO

Wakisimulia maisha ya marehemu, majirani hao walisema marehemu kabla ya kupatwa na umauti, alikuwa katika taratibu za vikao vya harusi ambavyo vilishaanza hivyo vikao hivyo vikabadilika na kuwa mikakati ya mazishi.

“Kabla ya tukio hilo, marehemu alikwenda kwao Moshi mkoani Kilimanjaro wiki moja iliyopita na mchumba’ke (Stanley) kwa lengo la kutambulishana na mikakati ya ndoa kupamba moto kwani ilikuwa ifanyike siku chache kabla ya tukio hilo la kusikitisha.

“Walipotoka Moshi walikwenda Tanga kwa upande wa mwanaume kwa lengo hilohilo la utambulisho na tulijua anarudi nyumbani leo (Jumanne) hapa alipopanga lakini cha kushangaza tulipigiwa simu na kwenda kukuta msiba,” alisema jirani.

MAZISHI

Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo hadi tunakwenda mitamboni, taratibu za mazishi zilikuwa zikiendelea na ilielezwa kuwa wamepanga kuusafirisha mwili wa marehemu nyumbani kwao Moshi.

KAMANDA WA POLISI

Gazeti liliwasiliana na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Dar, ACP Camillus Wambura ambaye alikiri kupokea taarifa za tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi ili kujua aliyehusika na mauaji hayo.

gpl

0 comments:

-