Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema hana
mpango wa kuwahoji Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na
chama hicho kwa sababu ya misimamo yao inayokinzana na miongozo ya
chama, kwa kuwa anawafahamu wote kwa majina na idadi yao haizidi kumi.
Kauli
hiyo ya Kinana inafuatia taarifa zilizoripotiwa na gazeti hili hivi
karibuni kuwa, CCM kimeanza kuwahoji baadhi ya wabunge wake, ambao ni
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu ya kupingana na maelekezo
ya chama hicho kuhusu Muundo wa Serikali mbili.
"Sisi
(CCM) hatuhoji mtu kwa sababu ya kuwa na msimamo tofauti, kwani hawa
wenye msimamo tofauti na chama hawazidi kumi ama siyo zaidi ya 15,"
alisema Kinana na kuongeza;
Kwa
mujibu wa habari hiyo, wajumbe waliohojiwa ni wale wanaotokana na Ubunge
wa Jamhuri ya Muungano na ambao wanataka Muundo wa Serikali tatu. "Ni
kweli hata mimi niliitwa na akaniambia (mwakilishi wa chama) ametumwa
aniletee ujumbe kuwa niko kwenye orodha ya watu 90 na nikiendelea na
msimamo wangu nitachukuliwa hatua," alieleza mmoja wa wajumbe waliodai
kuwa wamehojiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Maelezo ya Kinana
Kinana
aliliambia gazeti hili kuwa, kulingana na muundo wa chama hicho tawala,
viongozi wanaoweza kuwahoji watu ni yeye Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti,
Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa chama Taifa.
"Tena tunafanya hivyo kwenye vikao maalumu na kwa sababu ambazo
haziwezi kuwa siri."
Kinana
alieleza kuwa taarifa kwamba CCM imewahoji watu 90 kutokana na kuwa na
misimamo tofauti na chama hicho kuhusu Serikali mbili na kura ya wazi,
siyo za kweli na anaamini imesambazwa na watu kwa malengo yao binafsi.
Kinana anafafanua kuwa CCM kama chama kikubwa nchini chenye wafuasi
karibu nchi nzima, hakiwezi kudhibiti mitizamo ya watu na kimsingi
tofauti za mitazamo ndiyo msingi wa demokrasia.
Novemba
20 mwaka 2012 akizungumza katika kipindi cha Jenerali on Monday
kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Kinana alitoa
onyo kwa makada wasaliti kuwa atasimamia utekelezaji wa uamuzi wa
Halmashuari Kuu ya CCM (Nec) ya kuwabaini na kuwaondoa viongozi
wanaokwenda kinyume na matakwa ya chama na kukipaka matope.
Kura ya wazi na Serikali mbili
Katika
hatua nyingine, Kinana alizungumzia msimamo wa chama hicho wa kura ya
siri na muundo wa Serikali mbili, akieleza kuwa siyo jambo la ajabu,
kwani katika mchakato wa kutunga katiba, kila kundi lina maoni na
mtazamo wake na kuutetea kwenye mijadala.
"Wanaosema
kuna vyama havina msimamo pale bungeni ni waongo. Siyo vyama tu, kila
kikundi kina msimamo unaotokana na uchambuzi wao wa hali ya siasa nchini
na wanachofikiri kina masilahi kwa nchi na watu wanaofuata mtazamo wao.
Hawawezi kuniambia kama Lipumba (Profesa Ibrahim) na Mbowe (Freeman),
hawana wanachosimamia kwenye mjadala huo wa Bunge Maalumu," alisema na
kusisitiza:
"Watanzania
wasitarajie miujiza, lazima mivutano ya aina hiyo iwepo, kwani kila
kundi linajitahidi kupenyeza mawazo yake na wanaoitetea misimamo hiyo ni
watu. Kikubwa hapa sasa ni uvumilivu, watu wavumiliane na wazungumze
kwa hoja na mwisho wa yote wafikie mwafaka."
Alipoulizwa
kama ni kweli CCM imekuwa ikiwashinikiza wajumbe wake kusimamia matakwa
ya chama hicho, alijibu "Siyo CCM tu, CUF wanakutana na Chadema
wanakutana, tena kila siku. Hili ni jambo la kawaida."
Anasema
tatizo siyo chama kuwa na msimamo, bali chama kutokukubali kubadili
misimamo yake hata kama haikuwa sawa. Unaweza kuwa na msimamo wako,
lakini ukaja mbele ya wenzako, ukagundua kuwa hauko sahihi, ikifikia
hapo unapaswa kulegeza kamba ili uingize mawazo ya wenzako pia kwenye
hoja zako, alisema.
Wito kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba
Kinana
ametoa wito kwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba akiwataka watambue
kuwa Tanzania siyo nchi ya kwanza kutengeneza katiba.
Alisema
zipo nchi nyingi duniani, ikiwamo India, Indonesia, Columbia, Kenya na
Pakistan ambazo zilitumia muda mrefu zaidi kutunga katiba zao.
"Sisi
kutumia majuma matatu kutengeneza kanuni za kuongoza Bunge Maalumu la
Katiba, ni hatua nzuri tunayopaswa kujivunia," alisema.
Kinana
aliendelea kueleza kuwa pamoja na tofauti zinazojitokeza katika mijadala
ya Bunge hilo Maalumu, makundi yanayounda Bunge hilo yanapaswa kutambua
utaifa na uzalendo na ikilazimika waache tofauti zao ili wawe na
mwelekeo wa pamoja katika kufikia mwafaka unaokusudiwa.
"Kwa hali
hiyo pamoja na tofauti zetu, tusiondoke kwenye lengo. Mimi naamini
katiba tunayoitaka itapatikana ila safari ya kuipata ni ndefu na ngumu."
0 comments:
Post a Comment