Saturday, December 28

 
 
HUU ni msimu wa sikukuu! Juzi, tumesherehekea Sikukuu ya Krismasi na sasa tunaelekea Mwaka Mpya 2014. Kwa nguvu za Mungu tutafika salama. Ndugu zangu, hebu tutafakari vizuri kuhusu mwaka uliopita na kuangalia cha maana tulichofanya kwa wenzi wetu. Tuliwaumiza au tuliwapa furaha? Je, kupitia kona hii matatizo yameondoka, yamepungua au yameongezeka?  Nimeandika mada nyingi ambazo zimewagusa watu wengi. Ujumbe wenu na simu mlizopiga zinaonyesha jinsi kona hii inavyosomwa na watu wengi, tena makini.
Kwa vile tunakaribia kumaliza mwaka na kuanza mwingine mpya, basi napenda kuwapa kazi ya kufanya utafiti kuhusiana na mwenendo mzima wa maisha yenu ya kimapenzi.  Huu ndiyo muda muafaka wa kujichambua mwenyewe ulibeba vipi uhusiano ndani ya penzi lako. 
Katika muda wote kulikuwa na migongano, je, chanzo chake nini? Kama ni wewe ni muda wako wa kujirekebisha ili usiwe chanzo cha matatizo ya kila siku.
Ni makosa mtu kurudia kosa moja kila mara, mwanadamu anayejitambua hujifunza kupitia lile linalokemewa sana na mwenzake, japokuwa unapenda kulifanya. 
Sifa kubwa ya mwanadamu ni kufikiri kabla ya kutenda, siku zote mapenzi ni kusikilizana, kufarijiana na kubembelezana. Bila shaka mwaka huu unaomalizika kuna mambo yalitokea hadi kufikia hatua ya kutishia kuvunja ndoa au uhusiano wenu.
Mwaka unaisha, umekaa na kujiuliza tatizo nini? Umejichunguza na kujua labda wewe ndiye chanzo? 
Mmeukaribisha mwaka, mmekaa kama wanandoa au wapenzi kumaliza tofauti zenu? 
Kama hamjakaa kujadili mwenendo mzima wa uhusiano wenu kwa mwaka mzima hamjachelewa. Hebu kupitia makala haya kaeni chini na kuchambua matatizo yote yaliyowakwaza sana.
Tafuteni sehemu tulivu ili kupata nafasi ya kuzungumza kwa kujiamini. Sehemu hii haitakiwi mmoja kujiona yupo juu ya mwenzake au ubishi kwa kile ambacho kimemgusa.
 

Mazungumzo yenu yawe ya kirafiki, kosoaneni kwa sauti za kawaida, ondoeni jazba kwani muda huo hauna nafasi. Uwe mwepesi kukubali kosa na kuomba msamaha. Kwa vile nia yenu ni kujenga, hakikisheni yote yaliyowakwaza mwaka uliopita hamyapi tena nafasi. Jiepusheni kuwa chanzo cha maumivu ya wenzenu, umeamua huyo awe wako wa kufa na kuzikana kwa nini muumizane? Sawa, mwanadamu ana upungufu,  basi makosa yako yasiwe mazoea kwa vile tu upo juu ya mwenzako.
Mapenzi hayaangalii cheo, fedha wala uzuri wa sura na umbile, bali kujitoa kwa ajili ya mwenzako.
Jutia makosa uliyofanya mwaka huu na uanze upya mwaka ujao.
 

Anza mwaka ukiwa makini sana na kumfanya mpenzi wako asahau maumivu ya mwaka jana. Muahidi mpenzi wako kuwa mwaka huu utakuwa sehemu ya furaha yake ya kila siku, kama utakwenda tofauti basi utakuwa msaliti. 
Kiapo hiki si cha mtu mmoja bali kiwe cha wote. Kama kweli unayosema yanatoka moyoni na kuwa tayari kutorudia yaliyomkwaza mwenzako mwaka huu unaoishia, basi mwaka ujao utakuwa wa furaha na amani.  Nakutakieni mwaka mpya wenye mapenzi ya dhati, kila mmoja awe sehemu ya furaha ya mwenzake.


0 comments:

-