Tuesday, October 29

KATIKA uhusiano wa kimapenzi hakuna kitu kinachouma kama kusikia mpenzi wako uliyempa nafasi kubwa kwenye moyo wako anatembea na mtu mwingine. Licha ya kwamba ni kitu kinachoumiza sana, bado tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu wakiwasaliti wenza wao tena wakati mwingine waziwazi.
Aidha, wapo ambao wanafanya usaliti kwa kujificha sana kiasi kwamba wenzao wanaamini hawasalitiwi.
Huko nyuma utakumbuka nilishawahi kuzungumza kwamba, unapoingia kwenye uhusiano na mtu ambaye moyo wako umemzimikia, hutakiwi kuwa na mashaka naye.

Muamini na weka akilini mwako kwamba hawezi kukusaliti. Kwa kufanya hivyo maisha yako yatakuwa ni yenye amani siku zote.
 Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, tumekuwa tukiwashuhudia marafiki, ndugu na hata majirani zetu ambao tunawaona wametulia wakiwasaliti wenza wao kila kukicha.
Wapo wake za watu ambao tumekuwa tukiwaamini kuwa wametulia lakini siku moja tunawaona wakiingia gesti na wanaume wengine.
 Achilia mbali hilo, wewe unayesoma makala haya unaweza kuwa na rafiki yako ambaye unajua fika ana mtu wake lakini unashangaa anampa nafasi mtu mwingine na wanakuwa wakikutana kwa siri huku wewe ukiambiwa iwe siri yako.
Binafsi kuna dada mmoja ambaye namheshimu sana, ni jirani yangu ana mume wake ambaye inaonekana anampenda sana. Yule mume amekuwa na imani kubwa kwa mkewe kwamba hawezi kumsaliti lakini nimeshawahi kumuona na wanaume wengine na akanisihi sana nisimwambie mume wake. Na kweli siri hiyo imebaki moyoni mwangu hadi leo.
 Sasa katika mazingira hayo huwa nakaa na kujiuliza, wale wanaosema wanawaamini wapenzi wao kwa asilimia zote ujasiri wanaupata wapi? Hata kama ni suala la imani lakini siyo kwa mazingira tunayoishi sasa na sarakasi za usaliti zilivyo.
Utakuwa ukijilazimisha kuamini mpenzi wako hawezi kukusaliti lakini kuna wakati unajiwa na hisia kwamba anakusaliti ila hisia hizo unazipotezea ili kutojipa vidonda vya tumbo, si ndiyo ee?
Kikubwa nisisitize kwamba mapenzi ni imani. Ni sawa na kuamini kwamba Mungu yupo licha ya kwamba hujawahi kumuona. Vivyo hivyo, amini tu kwamba mpenzi wako anakupenda kwa dhati na hawezi kukusaliti licha ya kwamba kinyume chake pia ni sawa. Hiyo itakusaidia wewe kuendelea kuishi maisha ya furaha na amani.
Hivi ni wanaume wangapi ambao wake zao wanagawa penzi nje ya ndoa lakini waume zao hawajui na wanawaamini kupita maelezo? Ni wanawake wangapi ambao waume zao ni viwembe kwelikweli lakini wake zao wanawaamini kupindukia?
Tutambue tu kwamba, katika maisha kuna kitu kuridhika. Unapokuwa na mtu ambaye anakupa kila aina ya furaha maishani mwako bila kuonesha tabia zozote zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, huyo mpende, mheshimu na muamini.
Hata kama kuna uwezekano wa yeye kuwa anaficha makucha yake na kuyachomoa pale anapokuwa mbali na wewe, kwa sababu huna uhakika na hujawahi kumuona, chukulia kwamba yeye ni msafi kisha yaache maisha yenu yaendelee kuwepo.

0 comments:

-