Wednesday, August 21

             
 
Awali ya yote niwasalimuni wapenzi na wasomaji wa blog hii ya kevylarity.blogspot.com

Ndugu zangu, sasa turejee katika mada yetu ya leo. Nazungumzia mambo muhimu ambayo vijana wa sasa wanatakiwa kuyazingatia wakati wanatafuta pumziko la kweli. Upendo wa kweli si jambo dogo. Kumpata mwenzi wa maisha si maigizo!

Inahitaji muda na kutafiti kwelikweli. Unajua suala la kuoa na kuolewa ni agizo la Mungu mwenyewe, kwa maneno mengine ni moja ya hatua za maisha ya binadamu. Vitabu vitakatifu vimeandika juu ya ndoa. Lakini katika kufanya uchaguzi wa nani atafaa kuwa wako wa maisha ni lazima uchague mwenzi sahihi.
Zipo sifa nyingi za mwenzi sahihi, baadhi yake ni umpende, akupende, akuvutie (wewe), awe na tabia njema, akubalike, atoke familia yenye maadili n.k, lakini vijana wa siku hizi huhadaika zaidi na mvuto wa sura na maumbile ya mtu wakifanya kama kipimo kikuu cha anayefaa kuwa mwenzi wa maisha; wanakosea sana!
Uzuri wa nje pekee siyo kati ya sifa muhimu zaidi za kumfanya awe na sifa za kuwa mwenzi wako wa maisha. Mapenzi huanzia moyoni, jiridhishe kwanza ndipo ukubali kumwingiza katika moyo wako.
Kumbuka kuwa unapoamua kufunga ndoa na mtu ni ahadi ambayo mmeahidiana mbinguni na duniani, ni ahadi ambayo inapaswa kutenganishwa na kifo tu, siyo vinginevyo!
Kamwe usifanye majaribio katika mapenzi, mapenzi hayajaribiwi! Pia, lazima umchunguze kama penzi lake ni la dhati. Katika mada zangu mbalimbali nimekuwa nikiainisha sifa za mpenzi mwenye mapenzi ya dhati, lakini kwa kukukumbusha kidogo ni kwamba, anayekupenda huwa mvumilivu, anakusikiliza pia mwenye kuwajali ndugu, marafiki na jamaa zako, anayekuheshimu na kutambua thamani yako!
Anayetakiwa kuwa mwenzi wako wa maisha lazima awe makini na mwenye akili za kimaisha. Siyo lazima awe na elimu ya darasani, haijalishi ni mwanamke aliyekulia vijijini au mjini, lakini hapa tunaangalia uwezo wake wa kufikiri.
Hata hivyo inategemea wewe umepanga kuishi na mwanamke wa aina gani, lakini mwanamke ninayemzungumzia hapa ni yule mwenye uwezo wa kutosha wa kufikiri na kupambanua mambo.
Mwenye uwezo huu ni yule ambaye ukimwambia kibanda chako unachofanyia biashara kimevunjwa atakuwa na ushauri wa kukupa utakaokusaidia kuendesha maisha yenu na siyo kukulaumu au kuishia kukusikitikia bila kuwa na wazo la kukupa.
Kusikitika kwake hakumaanishi kuwa yupo pamoja na wewe, atakuwa pamoja na wewe pale atakapoonesha njia nyingine ya kukusaidia kujikwamua kimaisha.
Siyo kuishia mizinga kila siku, mara simu haina dola, mara mama Juma amepitisha vitenge anakopesha, lazima uangalie je, unapokwama anakuwa pamoja na wewe kifikra au ni kama mzigo wa mananasi? Hilo ni la kuzingatia sana katika maisha ya sasa.
Mwanamke wa aina hii unapaswa kumchunguza mapema ili usije ukaoa mzigo! Suala la uwezo wa kufikiri lina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya sasa, ni bora mkakosa mali lakini mkawa na uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo mbalimbali ya kimaisha.
Ni vyema pia ukajiridhisha, ni mwanamke wa ndoto yako? Unatakiwa kujiuliza juu ya uliyotarajia kwake, ni kweli unayapata yote? Hapa kuna vipengele viwili ndani ya hiki kimoja. Kwanza kabla ya uhusiano na pili, ndani ya uhusiano.
Nikianza na kabla ya uhusiano, hapa namaanisha kwamba, ana sifa zote ambazo ulikuwa unatarajia kwa mpenzi wako ajaye, ambaye ndiye huyo unayetarajia kuingia katika uhusiano naye. Ni kweli ana kila kitu kinachokuvutia kiasi kwamba hutathubutu kumsaliti?
Ukishajiridhisha na hilo, unaweza kuingia katika uhusiano lakini siyo kwa kasi kubwa, hapa namaanisha kwamba, unaingia katika kipindi cha urafiki ambacho huweki kila kitu wazi, hivyo katika kipindi hiki utaweza kujua kama unapata kile ulichotarajia.
Chunguza tabia zake kwa makini katika kipindi hiki, toka naye katika matembezi ya pamoja, huku ukiwa umemweka katika kipimo ambacho hata yeye mwenyewe atakuwa hafahamu. Lazima mwisho wa siku utaweza kugundua kwamba, chaguo lako lilikuwa sahihi au lah.
Lingine lenye msingi, anatakiwa awe mtu wa kujali. Hata kama ni mzuri kiasi gani, ana mvuto kiasi gani, anakubalika na marafiki zako kiasi gani, lakini vyote hivyo vinaweza kupoteza maana kama hataonyesha anavyojali thamani yako wewe kama mpenzi wake.
Ninapozungumzia kujali, nakuwa nimekwenda mbali zaidi, anavyojali familia yako, marafiki zako na hata wewe mwenyewe! Hutakiwi kuwa na mwanamke ambaye akili yake haiwazi chochote juu ya maisha. Mwanamke anapaswa kuwa makini, akili ziwe zinafanya kazi sawasawa na awe na mchango mkubwa wa mawazo kwenye familia.
Sifa ya mvuto wake, inaweza kuharibiwa na kukosa uchangamfu na unyenyevu. Mwanamke hata kama ni mzuri kwa kiwango gani, akipoteza sifa hizi, uzuri wake ni kama unakuwa umepungua. Uchangamfu huu uanzie kwako, asiwe mwanamke mkimya kupitiliza, hali ambayo inaweza kutafsiriwa kwamba anaringa!
Lakini pia, uchangamfu huu anatakiwa auonyeshe hata kwa rafiki zako pamoja na ndugu zako. Mwanamke mwema ni yule mwenye unyenyekevu kwa mumewe pamoja na ndugu zake.
Usidanganyike na uzuri wa nje, uzuri hauna maana ya ubora wa kuwa mke, siyo kila mwanamke anaweza kuwa mke! Mchunguze kwa makini, hakikisha ana sifa nilizozitaja na zingine muhimu, lakini kubwa kuliko yote, mwanamke huyo lazima awe anakupenda kwa mapenzi ya dhati. Sina shaka nimesomeka.tukutane muda mwingine tena.

0 comments:

-