Wednesday, August 28

MU hali gani mabibi na mabwana kwa kukutana tena kwenye safu yetu ya kujuzana mawili matatu kuhusu maisha yetu ya kila siku. Japo leo nilikuwa nimeandaa mada nyingine.

Lakini wakati najiandaa kuandika alikuja rafiki yangu wa karibu ambaye aliniletea matatizo mengi kutoka kwa mzazi mwenzake, ambaye wamezaa watoto wawili na wanaishi pamoja kama mke na mume.
Moja ya matatizo hayo ambayo yamejaa kwenye baadhi ya nyumba tunazoishi kwa mwanamke kukosa heshima wala woga kwa kufanya mambo kwa kujiamulia kama vile anajimiliki mwenyewe.

Mwenza wake amekuwa si mkweli mwenye matukio yanayoonesha kukosekana kwa uaminifu katika uhusiano wao. Amekuwa akitoka bila ruhusa na kurudi akiwa amelewa na aulizwapo huwa mkali.

Kibaya zaidi kilichomtokea siku ya jumamosi baada ya kukorofishana mwanamke yule alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu, kuwa mtoto mdogo wa mwaka mmoja siyo wake naye atafute wa kwake.

Nina imani hali hii imewakumba watu wengi ambao kila siku uendelea kuumia wakati wenzao wanaendelea kufurahia maisha. Matukio haya utokea wakati mwanamke anapokuwa na uhakika huna sauti kwake kwa kuonyesha udhaifu mbele yake.

Siwezi kuwa na upendeleo kwa kusema tabia hizi ni za wanawake peke yao, hata baadhi ya wanaume nao wapo wenye tabia hizi.

Kwa vile kona hii majibu yake huwa hayalengi upande mmoja, nilipenda nielezee kwa wote na kila mmoja asome kama ni yeye yamemkuta au yakitaka kukuta ufanyeje. Naanza kwa kusema ukiona vitu vyote hivi ujue ndani ya uhusiano au ndoa yako hakuna mapenzi bali kinachowaongoza ni mazoea. Na tatizo lilianza kama mzaha kwa kulifumbia macho kutokana na udhaifu mbele ya mwenzako kwa kuyaacha yote yaliyokwenda kinyume.

Nasema hivi kwa
maana gani?
Kila anayefuatilia kona hii atakubaliana na mada nilizozitoa kuhusu penzi la kweli na mnafiki wa mapenzi. Ila leo nataka niongezee kidogo ili tuelewe tupo wapi, tumetoka wapi na tunaelekea wapi katika mapenzi.

Utajiuliza inakuwaje mtu anakubali kufanyiwa hivi na kubakia kulalamika bila kuchukua hatua yoyote? Ukiona mtu au ukijiona upo hivi basi ujuwe wewe ni mtumwa wa mapenzi kwa kuongozwa na mapenzi na si wewe kuyaongoza.
Mtumwa wa mapenzi yukoje?

Mtumwa wa mapenzi ni yule anayependa kwa kumuona mpenzi wake ni mzuri na hawezi kumpenda mwingine kuliko yeye. Na hii utokea kwa kuamini kumpata ilikuwa ni bahati na wala si uwezo wako binafsi. Ukifikia hatua hii hata kumkanya kwa baya huwezi.

Watu wa aina hii huburuzwa na mapenzi kwa mpenzi wake kufanya jambo lolote bila woga kwa kuamini mpenzi wake anampenza kupindukia yaani ‘hageuzi’. Watu hawa huumia zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi. Uamini wakiachwa ndiyo mwisho wao wa kupenda au kupendwa. Napenda kusema haya machache ili usiwe mtumwa wa mapenzi:

Kwanza: Unatakiwa wewe ndiye uwe dereva wa kuyaongoza mapenzi siyo yenyewe yakuongoze.
Pili: Unatakiwa uwe na maamuzi sahihi ya moyo wako hasa panapotokea kufanyiwa kosa la makusudi kwa kulikemea kwa nguvu zote.

Tatu: Usikubali mpenzi wako akuumize kwa sababu unampenda kwa vile mapenzi ni kupendana kufarijiana na si kuumizana au kutesana.

Nne: Angalia katika mapenzi yako nini kimezidi, faida au hasara, chukua kilichozidi.
Tano: Jiamini kuwa kupenda au kupendwa kwako si bahati
Sita: Muweke chini mpenzio na kumueleza matatizo yake ambayo yanakwenda kinyume na watu waliokubaliana kuishi pamoja, kama hata kuwa muelewa, tafuta usuluhisho kwa watu mbalimbali wenye busara na ikishindikana ni wajibu wako wa kulivunja penzi.

Hapa naomba nieleweke kulivunja penzi iwe suruhisho la mwisho kabisa kama hakutapatikana suruhu ya aina yoyote. Na kulivunja penzi hakikisha umekubaliana na moyo wako. Jiepushe na kumkumbuka aliyeachana naye ili asiendelee kukuumiza. Siku zote adui ya moyo yako hawezi kupata nafasi moyoni mwako.

Mwisho: Jipange vizuri kabla ya kuanzisha penzi jipya ili usirudie kosa la awali. Na mwisho kabisa napenda kuwakumbusha wanawake wazuri wote au wanaume wenye fedha kuwa wakati ukuta na hakuna marefu yasiyo na ncha. Samahani kwa kosa la makusudi ni unafiki, samahani siku zote ni uungwana lakini haipunguzi machungu.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

0 comments:

-