Tuesday, August 13

Maisha ya binadamu ili yaweze kutawaliwa na furaha na amani ni lazima suala la mapenzi lipewe kipaumbele. Wakutane wawili wanaopendana kwa dhati na wanaodhihirishiana hivyo. Hapa namaanisha kwamba, watu hawa wapendane kutoka katika mioyo yao na si mapenzi ya mdomoni ya ‘I love you, I love you too’, hapana!
Tofauti na hivyo, sasa hivi tunashuhudia aina za mahusiano ya ajabu ambayo yanadhihirisha wazi kwamba, hakuna mapenzi bali watu wanapotezeana muda tu.

Katika hili sizungumzii walio katika uhusiano wa kawaida tu, namaanisha pia wale waliofikia hatua ya kuoana. Wapo walioingia katika ndoa lakini ukijaribu kufuatilia namna wanavyoishi utabaini kuwa wameoana kwa sababu tu imetokea hivyo lakini hakukuwa na mapenzi ya dhati.

Ndiyo maana kila siku tunashuhudia watu waliooana kwa mbwembwe na wakaahidiana kudumu milele wakiachana. Wengine hawaachani lakini tunaona jinsi wanavyokorofishana kila siku na kufikia hatua ya kupigana na kuumizana. Haya yote yanatokea kwa sababu, penzi lililokuwepo katikati yao halikuwa la dhati bali lilikuwa ni la kinafiki tu.

Wapo watu wengi ambao sasa hivi wapo katika mapenzi ya kinafiki na hata wewe unayesoma makala haya unaweza kuliona hili. Watu ni wapenzi au ni mke na mume, mbele za watu wanaonekana wanapendana sana kiasi cha wenzao kuwaonea donge lakini cha kushangaza watu hao hao wakiingia ndani hugeuka paka na chui, ugomvi kila wakati, matusi mpaka ya nguoni.

Yaani ni watu ambao hawaishi migogoro lakini kwa wewe mgeni ukiingia ndani kwao utakuta wanakuonesha tabasamu la kutengeneza, mapenzi ya kujifanyisha. Jamani kuwa katika aina hii ya penzi siyo unafiki?

Achilia mbali hilo, wapo watu ambao leo wanadai wanapendana kwa dhati lakini kesho unawakuta wamekorofishana mpaka mmoja wao anaamua kumweleza mwenzake kwamba bora waachane. Wanafikia hatua ya kutukanana, kupigana mpaka kuumizana lakini baada ya muda wanaombana msamaha, wanarudi tena penzini.

Sisemi kwamba ni unafiki wapenzi kukorofishana na kuombana msamaha na kusameheana, unafiki ninaouona hapa ni ule wa wapenzi kila wakati kutifuana na kufikia hatua ya kila mmoja kuona hayuko na mtu sahihi lakini baada ya muda, watu hao hao wanaondoa tofauti zao na kuendelea na maisha yao.

Mbaya zaidi ni kwamba, hata pale wanaporudiana mmoja kama siyo wote kiwango cha mapenzi hupungua. Labda katika hili niwafahamishie tu kwamba, unapokuwa ni mtu wa kumliza mpenzi wako kila mara, jua kwamba unapunguza kiwango cha yeye kukupenda.

Ndiyo maana ukichunguza sana unaweza kukuta mtu ambaye amekuwa ni wa kusalitiwa kila siku na mpenzi inafika wakati anaamua kumuacha mtu huyo licha ya kwamba alikuwa anampenda, kwa sababu ya maudhi hata mapenzi kwake yameshapungua.

Ninachotaka kukisema hapa leo ni kwamba, tuachane na mapenzi ya kinafiki. Kama kweli unampenda mpenzi wako epuka kumfanyia mambo ambayo yatamfanya ajiulize mara mbili mbili kama kweli unampenda.

Ndiyo maana ukiona mpenzi wako mmekuwa pamoja muda mrefu lakini leo hii anakuuliza swali la; Hivi mpenzi wangu unanipenda kweli? Tambua kuwa ameshaanza kuona dalili kwamba penzi lako kwake limechuja.

Tuoneshane mapenzi ya kweli kwa kuepuka kuwakwaza wapenzi wetu, tunawafanye kila siku iendayo kwa Mungu iwe ni ya furaha kwao. Kosa unalomfanyia mpenzi wako leo ukamuumiza, hakikisha halijirudii tena.

Hata kama utamkosea kesho basi liwe kosa lingine na siyo lile la jana. Endapo utakuwa ni mtu wa kumkwaza mpenzi wako kwa makosa yale yale itadhihirisha kwamba penzi lako kwake ni la kinafiki.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo

0 comments:

-