MU hali gani mabibi na mabwana kwa kukutana tena kwenye
safu yetu ya kujuzana mawili matatu kuhusu maisha yetu ya kila siku.
Japo leo nilikuwa nimeandaa mada nyingine.
Lakini wakati
najiandaa kuandika alikuja rafiki yangu wa karibu ambaye aliniletea
matatizo mengi kutoka kwa mzazi mwenzake, ambaye wamezaa watoto wawili
na wanaishi pamoja kama mke na mume.
Moja ya matatizo hayo ambayo
yamejaa kwenye baadhi ya nyumba tunazoishi kwa mwanamke kukosa heshima
wala woga kwa kufanya mambo kwa kujiamulia kama vile anajimiliki
mwenyewe.
Mwenza wake amekuwa si mkweli mwenye matukio
yanayoonesha kukosekana kwa uaminifu katika uhusiano wao. Amekuwa
akitoka bila ruhusa na kurudi akiwa amelewa na aulizwapo huwa mkali.
Kibaya
zaidi kilichomtokea siku ya jumamosi baada ya kukorofishana mwanamke
yule alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu, kuwa mtoto mdogo
wa mwaka mmoja siyo wake naye atafute wa kwake.
Nina imani hali
hii imewakumba watu wengi ambao kila siku uendelea kuumia wakati wenzao
wanaendelea kufurahia maisha. Matukio haya utokea wakati mwanamke
anapokuwa na uhakika huna sauti kwake kwa kuonyesha udhaifu mbele yake.
Siwezi kuwa na upendeleo kwa kusema tabia hizi ni za wanawake peke yao, hata baadhi ya wanaume nao wapo wenye tabia hizi.
Kwa
vile kona hii majibu yake huwa hayalengi upande mmoja, nilipenda
nielezee kwa wote na kila mmoja asome kama ni yeye yamemkuta au yakitaka
kukuta ufanyeje. Naanza kwa kusema ukiona vitu vyote hivi ujue ndani ya
uhusiano au ndoa yako hakuna mapenzi bali kinachowaongoza ni mazoea. Na
tatizo lilianza kama mzaha kwa kulifumbia macho kutokana na udhaifu
mbele ya mwenzako kwa kuyaacha yote yaliyokwenda kinyume.
Nasema hivi kwa
maana gani?
Kila
anayefuatilia kona hii atakubaliana na mada nilizozitoa kuhusu penzi la
kweli na mnafiki wa mapenzi. Ila leo nataka niongezee kidogo ili
tuelewe tupo wapi, tumetoka wapi na tunaelekea wapi katika mapenzi.
Utajiuliza
inakuwaje mtu anakubali kufanyiwa hivi na kubakia kulalamika bila
kuchukua hatua yoyote? Ukiona mtu au ukijiona upo hivi basi ujuwe wewe
ni mtumwa wa mapenzi kwa kuongozwa na mapenzi na si wewe kuyaongoza.
Mtumwa wa mapenzi yukoje?
Mtumwa
wa mapenzi ni yule anayependa kwa kumuona mpenzi wake ni mzuri na
hawezi kumpenda mwingine kuliko yeye. Na hii utokea kwa kuamini kumpata
ilikuwa ni bahati na wala si uwezo wako binafsi. Ukifikia hatua hii hata
kumkanya kwa baya huwezi.
Watu wa aina hii huburuzwa na mapenzi
kwa mpenzi wake kufanya jambo lolote bila woga kwa kuamini mpenzi wake
anampenza kupindukia yaani ‘hageuzi’. Watu hawa huumia zaidi ya
kung’olewa jino bila ganzi. Uamini wakiachwa ndiyo mwisho wao wa kupenda
au kupendwa. Napenda kusema haya machache ili usiwe mtumwa wa mapenzi:
Kwanza: Unatakiwa wewe ndiye uwe dereva wa kuyaongoza mapenzi siyo yenyewe yakuongoze.
Pili: Unatakiwa uwe na maamuzi sahihi ya moyo wako hasa panapotokea kufanyiwa kosa la makusudi kwa kulikemea kwa nguvu zote.
Tatu:
Usikubali mpenzi wako akuumize kwa sababu unampenda kwa vile mapenzi ni
kupendana kufarijiana na si kuumizana au kutesana.
Nne: Angalia katika mapenzi yako nini kimezidi, faida au hasara, chukua kilichozidi.
Tano: Jiamini kuwa kupenda au kupendwa kwako si bahati
Sita:
Muweke chini mpenzio na kumueleza matatizo yake ambayo yanakwenda
kinyume na watu waliokubaliana kuishi pamoja, kama hata kuwa muelewa,
tafuta usuluhisho kwa watu mbalimbali wenye busara na ikishindikana ni
wajibu wako wa kulivunja penzi.
Hapa naomba nieleweke kulivunja
penzi iwe suruhisho la mwisho kabisa kama hakutapatikana suruhu ya aina
yoyote. Na kulivunja penzi hakikisha umekubaliana na moyo wako. Jiepushe
na kumkumbuka aliyeachana naye ili asiendelee kukuumiza. Siku zote adui
ya moyo yako hawezi kupata nafasi moyoni mwako.
Mwisho:
Jipange vizuri kabla ya kuanzisha penzi jipya ili usirudie kosa la
awali. Na mwisho kabisa napenda kuwakumbusha wanawake wazuri wote au
wanaume wenye fedha kuwa wakati ukuta na hakuna marefu yasiyo na ncha.
Samahani kwa kosa la makusudi ni unafiki, samahani siku zote ni uungwana
lakini haipunguzi machungu.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

No comments:
Post a Comment