WATU wengi wanapenda kuwa maarufu, wenye
uwezo na ushawishi katika jamii lakini hawafahamu wafanye nini kufikia
ndoto zao. Kuna wanaolazimika kufanya hata mambo machafu mfano kupiga
picha za utupu wakiamini zitawasaidia kujulikana.
Mfumo
wa kufanya kitu chochote ili uwe maarufu si mzuri; zipo mbinu za
kitaalamu ambazo mtu akizitumia anaweza kuwa maarufu na mwenye mafanikio
makubwa katika jamii. Nazo ni hizi hapa.
Hakikisha ujuzi wako haumfuniki mkuu wako au watu wengine
Unaweza
usiwe ujuzi pekee lakini hata uwezo wako wa kiakili, mali na uelewa.
Hakikisha hauutumii kwa majivuno kuonesha jinsi unavyowazidi wenzako
kazini, kwenye biashara, darasani hasa watu waliokuzidi cheo. Siku zote
hakikisha kuwa unawatanguliza wenzako, kuthamini mchango wao na kusifu
uwezo wao.
Kizuizi kikubwa kabisa kwenye maisha ya umaarufu, heshima
na mamlaka kwenye jamii ni kujiona bora kuliko wenzako, jambo
linalowafanya watu pamoja na uwezo wao washindwe kuheshimika na
kupendwa.
Usiwaamini mno marafiki, jifunze kuwatumia maadui zako.
Jihadhari
na marafiki, kwani wanaweza kukusaliti haraka zaidi kwani ni rahisi
sana kwao kukuonea wivu. Watu hao ni rahisi sana kubadilika na kuwa
katili. Ukianzisha uhusiano na mtu ambaye aliwahi kuwa adui yako,
utagundua kwamba atakuwa mwaminifu zaidi kwako kuliko rafiki, kwani
anakuwa anataka kukuthibitishia kwamba uhusiano wenu ni wa dhati. Kwa
kifupi, waogope zaidi marafiki zako kuliko maadui.
Katika safari ya
kuelekea kwenye kilele cha umaarufu na heshima, kuwa na maadui ni jambo
muhimu kwani husaidia kuongeza ari na huthibitisha uwezo wako hasa pale
inapotokea maadui zako kusalimu amri kwako.
Dhamira zako zifanye siri
Hakikisha
watu hawakuelewi kwa dhamira zako au sababu ya kile unachokifanya. Kama
hufahamu nini unataka kukifanya, ni dhahiri watakuwa hawana nguvu ya
kukufanya lolote. Hakikisha unawapotosha wasijue mipango yako na wakati
watakapofahamu dhamira yako, watakuwa wamechelewa kwani utakuwa tayari
umeikamilisha mipango hiyo.
Epuka kuwa mtu wa kuropoka juu ya
madhumuni yako ya maisha, utawapa nafasi wabaya wako kukuwekea vikwazo
vya kukuzuia usifike mahali ulipokusudia.
Usipende kuzungumza sana
Unapotaka
kuwavutia watu, punguza wingi wa maneno yako, kusema sana kunaweza
kuwafanya wanaokusikiliza wakakukinahi. Watu maarufu huweza kuwavutia
na kuwaogopesha watu kwa kusema maneno machache. Jinsi unavyozungumza
zaidi, ndivyo unavyojenga uwezekano wa kusema kitu cha kipumbavu
kitakachokudharaulisha.
Hakikisha unalinda hadhi
yako katika jamii
Hadhi
katika jamii ndiyo nguzo ya mamlaka. Kwa kutumia hadhi yako pekee
unaweza kuwaogopesha watu na ukafanikiwa mambo yako; lakini ukipotoka
tu, fahamu umeingia matatani na utashambuliwa kutoka pande zote.
Hakikisha hadhi yao inabaki imara.
Itaendelea wiki ijayo...
No comments:
Post a Comment